MACHI 11, 2013
Uturuki
Shirika la Umoja wa Mataifa Lasema Lazima Uturuki Iheshimu Dhamiri ya Raia Wake
Mamilioni ya Wakristo hukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yao—na nchi nyingi huheshimu uamuzi wao. Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ilitoa uamuzi kwamba raia wa Uturuki wanastahili kuwa na uhuru huo.
Katika uamuzi uliotolewa Machi 29, 2012, Kamati hiyo iliunga mkono uamuzi huo wa raia wawili wa Uturuki, Cenk Atasoy na Arda Sarkut. Wanaume hao wawili ni Mashahidi wa Yehova waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya imani yao ya kidini.
Bw. Atasoy na Bw. Sarkut walikuwa wametuma maombi mara nyingi kwenye ofisi za serikali ili kueleza kuhusu uamuzi wao unaotegemea dhamiri, na waliomba ikiwa wanaweza kufanya utumishi mwingine wa kiraia usiohusiana na jeshi. Hata hivyo, wanaume hao walishurutishwa sana wajiunge na jeshi. Jeshi lilipotisha kwamba lingefungua mashtaka dhidi ya chuo kikuu kilichokuwa kimemwajiri Bw. Sarkut kuwa mhadhiri msaidizi, alifutwa kazi.
Katika uamuzi wake, Kamati hiyo ilisema kwamba haki ya kukataa utumishi wa jeshi kwa sababu ya dhamiri “inalingana na haki ya mtu kuwa na uhuru wa kufikiri, kuwa na dhamiri, na dini,” maneno yanayotajwa katika Kifungu namba 18 cha Agano la Kimataifa Kuhusu Haki za Kiraia na za Kisiasa. Isitoshe, Kamati hiyo iliamua kwamba haki hiyo, “inamfanya kila mtu awe na ruhusa ya kutohusishwa katika utumishi wa lazima wa kijeshi iwapo utumishi huo haupatani na dini au imani ya mtu.”
Uamuzi huo umetolewa baada ya maamuzi mawili yanayofanana na huo yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu. Katika mojawapo ya maamuzi hayo, Mahakama hiyo iliamua kwamba “kukosa kuwa na utumishi wa badala ya utumishi wa jeshi nchini Uturuki kunavunja haki ambayo watu wanayo ya kukataa kufanya jambo kwa sababu ya dhamiri” inayopatikana katika Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.
Uamuzi wa kukataa kujihusisha katika jeshi kwa sababu ya dhamiri ulianza zamani wakati Ukristo ulipoanza. E. W. Barnes, aliandika hivi katika kitabu chake The Rise of Christianity: “Uchunguzi wenye kina wa habari yote inayopatikana [unaonyesha] kwamba, hadi wakati wa Marcus Aurelius [maliki Mroma kuanzia 161 hadi 180 W.K.], hakuna Mkristo aliyekuwa mwanajeshi; na hakuna mwanajeshi, ambaye baada ya kuwa Mkristo, aliendelea na utumishi wake wa kijeshi.”