JANUARI 25, 2022
AFRIKA KUSINI
Maofisa Nchini Afrika Kusini Wawapongeza Mashahidi wa Yehova kwa Kuwasaidia Viziwi
Vitabu Viwili Vingine vya Biblia Vyatolewa Katika Lugha ya Ishara ya Afrika Kusini
Nchini Afrika Kusini, mashirika ya kuwasaidia viziwi yamewashukuru Mashahidi wa Yehova kwa kuwasaidia viziwi kuboresha maisha yao kwa kuwaandalia video za hali ya juu katika Lugha ya Ishara ya Afrika Kusini (SASL). Wamefanya hivyo baada ya kutolewa kwa vitabu vya Wagalatia na Waefeso vya Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika SASL. Vitabu hivyo vilitolewa Novemba 15, 2021. Kufikia sasa vitabu kumi vimetolewa katika SASL. Inatarajiwa kwamba vitabu vingine vinne vitatolewa kufikia Aprili 2022. Vyote vinapatikana kwenye jw.org na kwenye programu ya JW Library Sign Language.
Minna Steyn, mwalimu na kiongozi wa Serikali ya Western Cape, alisema hivi kuwahusu Mashahidi: “Ninapenda sana kuwatazama wanaokalimani lugha ya ishara na ningependa kuwapongeza wao pamoja na tengenezo lenu kwa ishara za kiwango cha juu na ubora wa hali ya juu.”
Bongani Makama, msimamizi wa Shirikisho la Walemavu nchini Eswatini, alisema hivi: “Tunawapongeza Mashahidi wa Yehova kwa kuwawezesha viziwi na watu walio na matatizo ya kusikia kupata habari zinazofurahiwa na watu walio na uwezo wa kusikia.” Aliongezea hivi: “[Viziwi] wanastahili kuwa na Biblia katika lugha yao. Hiyo ndiyo sababu tunawapongeza Mashahidi wa Yehova kwa kuwaandalia viziwi vitabu hivyo vya Biblia katika lugha inayogusa mioyo yao. Tunasubiri kwa hamu kupata vitabu vyote 66 vya Biblia katika lugha ya ishara.”
Inakadiriwa kwamba watu 450,000 nchini Afrika Kusini wanatumia SASL. Kuna wahubiri 283 ambao ni viziwi nchini Afrika Kusini. Kwa sababu ya jitihada za Mashahidi, “watu wa namna zote” wanapata ujuzi sahihi wa kweli, kutia ndani viziwi katika eneo la ofisi ya tawi ya Afrika Kusini.—1 Timotheo 2:4.