Hamia kwenye habari

OKTOBA 16, 2017
ARMENIA

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatetea Haki ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Nchini Armenia

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatetea Haki ya Wanaokataa Kujiunga na Jeshi kwa Sababu ya Dhamiri Nchini Armenia

Oktoba 12, 2017, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi kwamba Mashahidi wa Yehova wanne nchini Armenia walikuwa wamefungwa isivyo haki kwa sababu walikataa kufanya utumishi wa badala ambao ulikuwa ukisimamiwa na jeshi. ECHR ilieleza kwamba vijana hao wanne walikuwa wamehukumiwa kimakosa kwa sababu Armenia ilikuwa imeshindwa kuwapa utumishi wa badala unaofaa.

Wahusika wa kesi ya Adyan na Wengine dhidi ya Armenia, ni Artur Adyan, Vahagn Margaryan, Harutyun Khachatryan, na Garegin Avetisyan, ambao walihukumiwa wakati wa majira ya kiangazi ya mwaka wa 2011 kutumikia kifungo cha miaka miwili na nusu gerezani. ECHR ilieleza kwamba mashtaka na hukumu waliyopewa vijana hao ilikuwa imekiuka haki yao ya uhuru wa dhamiri na dini kama inavyoonyeshwa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu. Armenia iliagizwa imlipe kila mmoja wao dola 14,200 za Marekani kama fidia kutokana na maumivu na mateso waliyokabili.

Vijana hao walihukumiwa muda mfupi baada ya Baraza Kuu la ECHR kutoa uamuzi katika kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia (2011), ulioeleza kwamba Mkataba wa Ulaya unalinda haki za wale wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. a Kwa kuwa haki hiyo imelindwa, Armenia ilihitaji kuwapatia utumishi wa badala wote wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Hata hivyo, utumishi wa badala uliokuwa ukitolewa na Armenia wakati huo ulikuwa haukidhi viwango vya kimataifa kwa sababu ulikuwa ukiongozwa na kusimamiwa na jeshi. Vijana hao wanne walikataa utumishi huo wa badala na wakafungwa kama walivyofungwa waabudu wenzao. Katika kesi ya Adyan, ECHR iliamua kwamba Armenia inapaswa kuwapa wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri “utumishi wa badala ambao hauhusiani na jeshi hata kidogo na wasipewe utumishi utakaowavunja moyo au unaoonekana kama adhabu.”

Baada ya vijana hao wanne ambao ni wahusika wa kesi ya Adyan kuachiliwa mwishoni mwa mwaka 2013, hatimaye Armenia ilitekeleza mkataba kwa kutoa utumishi wa badala wa kiraia ambao hausimamiwi wala kuongozwa na jeshi. Sasa, Mashahidi wa Yehova nchini Armenia ambao wanakataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri hawafungwi tena gerezani kwa kutii dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia na kukataa kufanya utumishi wa kijeshi. Wanathamini sana kupata nafasi ya kufanya utumishi wa badala wa kiraia unaofaa.

a Bayatyan dhidi ya Armenia [GC], na. 23459/03, ECHR 2011