Hamia kwenye habari

NOVEMBA 20, 2013
ARMENIA

Armenia Yawaachilia Huru Mashahidi Wote wa Yehova Waliofungwa Gerezani

Armenia Yawaachilia Huru Mashahidi Wote wa Yehova Waliofungwa Gerezani

YEREVAN, Armenia—Mnamo Novemba 12, 2013, Serikali ya Armenia iliwaachilia huru Mashahidi 14 waliosalia gerezani ambao walikuwa wamefungwa kwa sababu ya kukataa kujiunga na jeshi. Tangu Oktoba 8, 2013 jumla ya Mashahidi wa Yehova 28 waliokuwa wamefungwa gerezani kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, wameachiliwa huru. Hiyo inaonyesha kwamba nchi ya Armenia ambayo imekuwa ikipuuza haki za wale wanaokataa kujiunga na jeshi imeamua kubadili sera zake, sera ambazo zilisababisha vijana ambao ni Mashahidi wa Yehova wafungwe gerezani katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kwa mara ya kwanza sasa tangu mwaka wa 1993, hakuna Shahidi wa Yehova hata mmoja aliye gerezani nchini Armenia kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kabla ya kuwaachilia huru wafungwa hao mnamo Novemba 12, serikali ya Armenia ilikuwa imewaachilia huru Mashahidi wanane Oktoba tarehe 8 na 9. Jambo hilo liliwezekana kwa sababu walikuwa wamepunguziwa kifungo chao kwa miezi sita. Mashahidi wengine sita waliachiliwa huru Oktoba 24. Mashahidi hao sita walikuwa wa kwanza kufaidika kutokana na marekebisho ya Juni 8, 2013 katika sheria ya sasa ya Armenia ya utumishi wa badala wa kiraia. Marekebisho hayo yamewawezesha wale wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri kuchagua kufanya utumishi wa badala usiosimamiwa wala kuongozwa na jeshi badala ya kufungwa gerezani.

Zaidi ya Mashahidi 90 wameomba kujiunga na mpango huo mpya. Mnamo Oktoba 23 na Novemba 12, 2013, Tume ya Jamhuri ilipitia na kukubali maombi ya Mashahidi vijana 71 kati ya hao. Tume hiyo ilitangaza nia yake ya kusikiliza kesi zilizosalia baada ya muda mfupi.

David A. Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova katika makao yao makuu ya ulimwenguni pote huko New York, alisema: “Tunafurahi sana kuwa serikali ya Armenia imewaachilia huru vijana hao na kuwa suala hili la muda mrefu hatimaye limetatuliwa.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Armenia: Tigran Harutyunyan, simu +374 93 900 482