Hamia kwenye habari

ARMENIA

Maelezo Mafupi Kuhusu Armenia

Maelezo Mafupi Kuhusu Armenia

Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Armenia wameabudu kwa uhuru na kuendesha utendaji wa dini bila vizuizi vikubwa. Walisajiliwa rasmi Oktoba 2004.

Kufikia Oktoba 2013, changamoto kubwa ambayo Mashahidi walikabili nchini Armenia ni kutokuwa na utumishi wa badala wa kiraia unaofaa, kwa kuwa mpango uliowekwa na serikali ya Armenia ulisimamiwa na jeshi na ulihusisha adhabu kali. Tangu 1993, Mashahidi wengi vijana waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri walihukumiwa vifungo virefu gerezani na baadhi yao walivumilia hali ngumu sana. Hatimaye, Juni 8, 2013, Armenia ilirekebisha Sheria ya Utumishi wa Badala wa Kiraia ili ipatane na viwango vya Ulaya. Oktoba 23, 2013, Tume ya Jamhuri ya Armenia ilikubali kwa mara ya kwanza maombi ya utumishi wa badala wa kiraia ya Mashahidi wa Yehova 51. Mpango huo una mafanikio kwa kuwa unawaruhusu Mashahidi watumikie nchi yao wakiwa na dhamiri safi.

Licha ya maendeleo hayo, bado Mashahidi wa Yehova wanabaguliwa. Baadhi ya manispaa zinakataa kutoa vibali vya ujenzi wa majengo ya ibada ya Mashahidi, maofisa wa forodha wanatoza kodi kubwa ili kuruhusu machapisho yao yaingie nchini, na wapinzani wanasambaza habari za uwongo kuhusu Mashahidi wa Yehova kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Mashahidi wa Yehova wamepeleka kesi kwenye mahakama nchini humo na mahakama za kimataifa ili kutatua matatizo hayo.