Hamia kwenye habari

DESEMBA 3, 2012
ARMENIA

Armenia Yaagizwa Iwalipe Fidia Mashahidi 17 wa Yehova

Armenia Yaagizwa Iwalipe Fidia Mashahidi 17 wa Yehova

STRASBOURG, Ufaransa—Mnamo Novemba 27, 2012, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu iliamua kwamba ni lazima serikali ya Armenia ilipe Euro 112,000 (Dola 145,226 za Marekani) kama fidia na pia gharama za kesi baada ya kukiuka haki za Mashahidi 17 waliokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri yao.

Mwaka wa 2005, vijana 17 Mashahidi wa Yehova walikuwa wakifanya utumishi wa badala wa kijamii. Hata hivyo, walipotambua kwamba utumishi huo ulikuwa ukiongozwa na kusimamiwa na jeshi, hawangeweza kuendelea kufanya utumishi huo wakiwa na dhamiri safi, hivyo, wakaacha utumishi huo. Kwa sababu hiyo, walikamatwa na kushtakiwa. Baadhi yao walifungwa gerezani kwa miezi kadhaa kabla ya kupelekwa mahakamani, na mwishowe 11 kati yao walihukumiwa vifungo vya miaka miwili hadi mitatu gerezani.

Mahakama ya Ulaya iliamua kwamba mashtaka hayo ya jinai na vifungo hivyo havikuwa halali kwa sababu mnamo mwaka wa 2005, Armenia haikuwa na sheria yoyote iliyosema kwamba kuacha utumishi wa badala wa kijamii ni kosa la jinai. Mahakama hiyo ilisema kwamba serikali ya Armenia ilikiuka haki ya Mashahidi hao ya kuwa huru na kulindwa chini ya Kifungu Namba 5 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu. Ingawa baadaye serikali hiyo ilifutilia mbali mashtaka hayo ya jinai yasiyo halali na uamuzi wake wa kuwafunga Mashahidi hao 17, serikali ya Armenia ilikataa kuwalipa fidia kwa sababu ya kuwashtaki na kuwafunga kinyume cha sheria. Kwa hiyo, Mahakama hiyo iliagiza serikali ya Armenia iwalipe fidia kwa sababu ya kuwaharibia sifa na kulipia gharama za kesi.

Uamuzi huo unafuatana na uamuzi wa kesi nyingine tatu uliofanywa na Mahakama ya Ulaya ukishutumu serikali ya Armenia kuhusiana na suala la kutoshiriki katika utumishi wa kijeshi. Katika kesi hizo nne, wenye mamlaka katika serikali ya Armenia waliwatesa Mashahidi wa Yehova waliokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri yao na pia waliwatendea isivyo haki kama wahalifu hatari.

“Uamuzi wa Mahakama ya Ulaya umesaidia kukomesha ukosefu wa haki ambao Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakitendewa,” asema André Carbonneau, wakili wa Mashahidi hao. “Ushindi huo mfululizo dhidi ya Armenia katika Mahakama ya Ulaya ni onyo lililo wazi kwa nchi nyingine katika Baraza la Ulaya na pia nchi kama vile Eritrea, Korea Kusini, na nchini nyingine katika Asia ya Kati kuhusiana na haki ya Mashahidi wa Yehova ya kukataa utumishi wa kijeshi.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Armenia: Tigran Harutyunyan, simu +374 93 900 482