Hamia kwenye habari

Kushoto: Ndugu Kenneth Cook akitoa hotuba yenye kutia moyo ya Kimaandiko kwa ajili ya wale waliofanya kazi katika eneo la mandhari za kale. Juu kulia: Video ikirekodiwa katika studio ya ndani. Chini kulia: Video ikirekodiwa katika eneo la nje la mandhari ya kale

AGOSTI 26, 2022
AUSTRALIA

Kipindi cha 1 cha Mfululizo Habari Njema Kulingana na Yesu Kimepiga Hatua Kubwa

Kipindi cha 1 cha Mfululizo Habari Njema Kulingana na Yesu Kimepiga Hatua Kubwa

Agosti 12, 2022 sehemu ya kwanza ya matayarisho ya Kipindi cha 1 cha mfululizo wa video Habari Njema Kulingana na Yesu ilikamilishwa. Baada ya kukatizwa kwa muda fulani, sehemu ya pili ya matayarisho itaanza, na inatarajiwa kukamilika muda fulani mnamo Oktoba 2022.

Kama ilivyoripotiwa awali, Mei 20, 2022 ndipo akina ndugu walianza kurekodi mfululizo huo wa video Habari Njema Kulingana na Yesu. Walitumia maeneo ya ndani kurekodi sehemu mbalimbali. Wakati huo bado vibali fulani vilikuwa vikisubiriwa ili kujenga majengo ya utegemezaji wa kazi hiyo na pia ili kusimamisha maeneo ya nje yanayoonyesha mandhari za kale. Vibali hivyo vilipatikana Julai 15, 2022. Idara ya Ujenzi ya Ofisi ya Tawi ya Australasia ilikabidhi majengo hayo pamoja na eneo la kurekodia video kwa Kikundi cha Eneo cha Kutayarisha Video (RVT). Sasa majengo hayo yanaweza kutumiwa kikamili katika mradi wa kutayarisha video hizo.

Jengo linalotumiwa kutegemeza kazi ya idara ya Kikundi cha Eneo cha Kutayarisha Video (RVT). Jengo hilo lina eneo la jikoni, chumba cha kulia chakula, eneo la ofisi, na chumba cha kushughulikia nywele na mapambo. Wanyama watakaotumiwa katika video wanatunzwa katika zizi

Zaidi ya wajitoleaji 500 kutoka Australia na New Zealand walihusika katika ujenzi wa eneo hilo la kurekodia mandhari sahihi za kale lenye ukubwa wa mita 7,000 za mraba. Ndugu Russell Grygorcewicz, mratibu wa Halmashauri ya Ujenzi anasema hivi kuhusu ujenzi huo: “Ingawa tulikabili changamoto nyingi sana, tulijionea wazi uthibitisho wa msaada wa Yehova katika kukabiliana nazo. Bila shaka, yote hayo yalitimizwa kwa roho ya Yehova.”

Ndugu Ronald Curzan, msaidizi wa Halmashauri ya Ufundishaji, alikuwepo kwa muda mrefu wakati wa kurekodiwa kwa sehemu ya kwanza ya video hiyo. Alisema hivi: “Ushirikiano na urafiki miongoni mwa wajitoleaji wa ujenzi na familia ya Betheli umekuwa wenye kupendeza sana. Inapendeza kuona maeneo ya kurekodia yakianza kutumiwa kikamili baada ya miaka mingi ya matayarisho na ujenzi. Imegusa moyo sana kuona msaada mwingi sana kutoka kwa akina ndugu katika eneo lote la ofisi ya tawi. Bila shaka, mfululizo huu ulio na vipindi 18 unaoonyesha maisha na mafundisho ya Yesu utagusa mioyo ya watu duniani pote.”

Ndugu Kenneth Cook wa Baraza Linaloongoza, aliyekuwepo katika siku za mwisho za kurekodi Kipindi cha 1 alisema hivi: “Ni wazi kwamba mkono wa Yehova wenye upendo unaunga mkono mradi huu. Tunamshukuru Yehova pamoja na wote ambao wamehusika katika ujenzi wa maeneo ya kurekodia na pia katika kazi ya kurekodi kwa kujidhabihu kwao na kwa kazi yao ya upendo. Tunasali kwamba mfululizo huu wa pekee wa video utawasaidia watu wengi kumfuata Yesu kwa ukaribu zaidi na kumkaribia Yehova zaidi.”

 

Mwingilio wa eneo la mandhari za kale

Picha ya kutoka juu inayoonyesha sehemu fulani ya eneo la mandhari za kale

Zizi la kondoo (mbele) lililo nje ya eneo la mandhari za kale

Eneo la sokoni

Eneo la serikali