JANUARI 10, 2020
AUSTRALIA
Moto wa Msituni Waendelea Kuwaka Nchini Australia
Kwa kuwa mwaka huu umekuwa wenye joto zaidi na mkavu zaidi katika historia ya Australia, moto wa msituni unaendelea kuongezeka. Tangu Septemba 2019, moto mkubwa umekuwa ukitokea katika sehemu nyingi katika majimbo ya Australia. Huu ndio mwanzo tu wa kipindi ambacho moto huwaka katika sehemu nyingi nchini humo, lakini tayari kimekuwa kipindi kibaya sana. Victoria na New South Wales ambayo ni mikoa ya pwani na ya kusini-mashariki ndiyo iliyoathiriwa zaidi.
Hakuna ndugu au dada yeyote aliyekufa au kuumia, lakini nyumba nyingi ziliharibiwa, kutia ndani nyumba tisa ambazo ziliteketea kabisa. Kufikia sasa, zaidi ya ndugu na dada 700 wamelazimika kuhama makao yao. Familia nyingi za Mashahidi zimeamua kuhama maeneo yaliyoathiriwa kwa sababu ya moshi mwingi, ambao umefafanuliwa kuwa dharura ya afya ya umma. Wengi kati ya wale waliolazimika kuhama wamechagua kuishi na familia, marafiki, na wahubiri katika makutaniko ya karibu, ambayo hayajaathiriwa moja kwa moja na moto huo.
Ofisi ya tawi ya Australasia imeunda Halmashauri mbili za Kutoa Msaada ili kuwasaidia kiroho na wa kimwili. Waangalizi wawili wa mzunguko na washiriki wa Halmashauri ya Tawi wanafanya ziara za uchungaji na kuwatia moyo ndugu na dada katika maeneo yaliyoathiriwa. Ijapokuwa ndugu na dada wengi walioathiriwa na moto huo wamechoka sana, kimwili na kihisia, wengi wameshukuru sana kwa upendo wa Kikristo ambao ndugu zao wanaendelea kuwaonyesha.—1 Petro 2:17.