Hamia kwenye habari

Ndugu Seymur Mammadov amefungwa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri

OKTOBA 20, 2022
AZERBAIJAN

Azerbaijan Yakiuka Maamuzi ya ECHR na Kumfunga Seymur Mammadov kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi

Azerbaijan Yakiuka Maamuzi ya ECHR na Kumfunga Seymur Mammadov kwa Kukataa Kujiunga na Jeshi

Septemba 22, 2022, Mahakama ya Wilaya ya Goranboy nchini Azerbaijan ilimhukumu Ndugu Seymur Mammadov mwenye umri wa miaka 22, kifungo cha miezi tisa gerezani kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri. Alikamatwa muda mfupi tu baada ya kutangazwa kwa hukumu hiyo mahakamani. Hukumu hiyo inakiuka kwa njia ya moja kwa moja maamuzi mawili yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) yanayohusu nchi ya Azerbaijan.

Tangu mwaka wa 2019, ECHR imetoa hukumu mbili dhidi ya Azerbaijan—Mamedov and Others v. Azerbaijan na Mekhtiyev and Abilov v. Azerbaijan. Maamuzi hayo mawili yaliunga mkono haki ya Mashahidi wa Yehova ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu za kidini, na haki hiyo inategemea kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya.

Katika kesi zote mbili, serikali ya Azerbaijan ilikiri kwa ECHR kwamba ilikuwa imekiuka haki za ndugu zetu na ikasema iko tayari kulipa fidia kwa sababu ya madhara iliyowasababishia Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, serikali ya Azerbaijan imepuuza kabisa maamuzi hayo ya ECHR kwa kukiuka haki za Ndugu Mammadov.

Kwa mara ya kwanza, Seymur Mammadov aliitwa kwenye Huduma ya Serikali ya Uhamasishaji na Usajili wa Eneo la Goranboy Mei 4,2022. Aliwaeleza maofisa waliohusika kuhusu imani yake inayotegemea Biblia na akaomba apewe utumishi wa badala wa kiraia. Maofisa hao walikataa ombi la Seymur. Licha ya hali hiyo, Ndugu Seymur alishikamana na imani yake.

Kwa sasa, Seymur amefungwa katika jiji la Ganja. Licha ya kukabili hali ngumu, Seymur anaendelea kudumisha mtazamo mzuri. Anasema kwamba amefaulu kuzungumza na wafungwa 30 hivi kuhusu imani yake. Hata anasema kwamba baadhi yao wameonyesha upendezi katika ujumbe wa Biblia.

Wakili wa Seymur amekata rufaa. Tunatumaini kwamba Mahakama ya Rufaa ya Ganja itafanya uamuzi ulio wa haki na kumwachilia ndugu yetu kutoka gerezani.

Hakuna shaka yoyote kwamba Yehova ataendelea kumsaidia Seymur anapokabiliana na jaribu hili.​—Isaya 43:2.