Hamia kwenye habari

DESEMBA 24, 2020
AZERBAIJAN

Hukumu za Hivi Karibuni Zilizofanywa na ECHR Zimeimarisha Uhuru wa Ibada Nchini Azerbaijan

Hukumu za Hivi Karibuni Zilizofanywa na ECHR Zimeimarisha Uhuru wa Ibada Nchini Azerbaijan

Katika mwezi wa Oktoba na Novemba 2020, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa hukumu kadhaa zinazounga mkono Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan. Kesi zilizohusika ni za Gridneva v. Azerbaijan, Sheveli and Shengelaya v. Azerbaijan, Jafarov v. Azerbaijan, na Tagiyev v. Azerbaijan. Hukumu hizo za ECHR zinaimarisha haki ya kisheria ya ndugu zetu ya kuhubiri, kukutanika pamoja ili kuabudu, na kuingiza machapisho nchini Azerbaijan.

Kesi hizo zilipelekwa Mahakamani mwaka wa 2011 na 2012. Kesi za Gridneva v. Azerbaijan na Sheveli and Shengelaya v. Azerbaijan zinahusu vitendo vya maofisa wa usalama kuvamia ndugu zetu katika mikutano au kuzuia kazi yetu ya kuhubiri. Kesi za Jafarov v. Azerbaijan na Tagiyev v. Azerbaijan zinahusu pindi ambazo serikali ilikataa au iliweka vizuizi vya kuingiza machapisho yetu kadhaa.

Kwa kupendeza, katika kesi tatu kati ya kesi hizo nne (Gridneva v. Azerbaijan, Jafarov v. Azerbaijan, na Tagiyev v. Azerbaijan), Azerbaijan ilikiri kwamba ilivunja haki za ndugu zetu na ikakubali kulipa fidia ya jumla ya euro 10,500 (sawa na dola 12,880 za Marekani).

Kesi ya Sheveli and Shengelaya v. Azerbaijan, ilihusisha wenzi wa ndoa waliokamatwa na kufukuzwa nchini kinyume na sheria baada ya kukutwa wakifanya kazi ya kutembelea makutaniko. ECHR iliagiza Azerbaijan iwalipe wenzi hao euro 3,000 (sawa na dola 3,680 za Marekani).

Katika hukumu hiyo, ECHR ilisema hivi: “Kukataza [wenzi hao] kusali au kushiriki imani yao ya kidini [hakupatani] na Makubaliano [ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu]. Kufanya hivyo ni sawa na kusema kwamba Azerbaijan hairuhusu dini ambazo hazijasajiliwa rasmi na serikali, na hilo litamaanisha kwamba Serikali inaweza kuamua kile ambacho mtu anapaswa kuamini.”

Katika miaka ya hivi karibuni, wenye mamlaka nchini Azerbaijan wamewatendea Mashahidi wa Yehova vizuri na wamelinda haki zao. Tunashukuru kwamba ndugu zetu wameungwa mkono na ECHR kupitia hukumu hizi. Zaidi ya yote, tunamshukuru Yehova Mungu, ambaye ni “kimbilio letu na nguvu zetu.”—Zaburi 46:1.