Hamia kwenye habari

JANUARI 5, 2021
AZERBAIJAN

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Yatetea Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Yatetea Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan

Desemba 15, 2020, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza hukumu mbili muhimu zinazotetea Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan. Kesi zilizohusika ni ya Rahima Huseynova v. Azerbaijan; na ya Saladdin Mammadov, Rashad Niftaliyev and Sadagat Abbasova v. Azerbaijan. Katika kesi zote mbili, Kamati hiyo iliamua kwamba nchi ya Azerbaijan iliwatendea Mashahidi wa Yehova kinyume na sheria za haki za kibinadamu na hivyo Kamati hiyo ikaagiza kwamba sheria za nchi hiyo zirekebishwe ili hali hiyo isitokee tena wakati ujao.

Kesi ya Rahima Huseynova v. Azerbaijan ilihusisha polisi katika mji wa Baku waliomfunga mahabusu Dada Rahima Huseynova katika mwezi wa Desemba 2014 kwa kosa la kuwaambia watu wengine kuhusu imani yake. Baadaye, mahakama ya wilaya ilimtoza faini ya Manat 1,500 za Azerbaijan (sawa na dola 882 za Marekani), kwa kuwa wakati huo Mashahidi wa Yehova hawakuwa wamesajiliwa katika jiji la Baku. a Alipokata rufaa, Mahakama ya Rufaa ya Baku iliunga mkono hukumu iliyotolewa mwanzoni na mahakama ya wilaya. Dada Huseynova aliamua kupeleka kesi yake katika mahakama ya kimataifa.

Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliamua kwamba nchi hiyo imevunja sheria ya kifungu cha 18(1) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR). Kamati hiyo iliagiza Azerbaijan imlipe fidia dada yetu. Inafurahisha kwamba katika taarifa yake iliyochapishwa, Kamati hiyo ilisema kwamba Azerbaijan “ina jukumu la kuchukua hatua zote muhimu ili kuepusha uvunjaji wa sheria hiyo wakati ujao, kuchunguza upya sheria za nchi, kanuni au utendaji wao wakiwa na kusudi la kuhakikisha kwamba haki za kibinadamu zilizotajwa kwenye kifungu cha 18 cha mkataba wa [ICCPR] zinatimizwa kikamili.”

Kesi ya Saladdin Mammadov, Rashad Niftaliyev and Sadagat Abbasova v. Azerbaijan inahusu kikundi cha akina ndugu na dada katika jiji la Ganja waliokutanika ili kujifunza Biblia katika nyumba ya Ndugu Saladdin Mammadov. Oktoba 2014, polisi walivamia mkutano huo mdogo, wakafanya msako katika nyumba hiyo na kisha wakachukua Biblia na vitu vingine. Ndugu Mammadov, Ndugu Rashad Niftaliyev, na Dada Sadagat Abbasova walipelekwa katika kituo cha polisi na wakawekwa kizuizini kwa zaidi ya saa sita. Baada ya siku mbili, walipelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Jiji la Ganja. Mahakama iliamua kwamba mkutano huo ulifanywa kinyume na sheria kwa kuwa kikundi hicho hakikuwa kimeandikishwa kuwa shirika la kidini katika jiji la Ganja. Mahakama ilimtoza kila mmoja wao faini ya Manat 2,000 za Azerbaijan (sawa na dola 1,176 za Marekani). Ndugu na dada hao walikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Ganja. Kwa kusikitisha uamuzi wa mahakama ya wilaya haukufutwa. Hivyo, wakakata rufaa kwenye Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kamati hiyo iligundua kwamba Azerbaijan ilivunja vifungu vingi vya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na kwamba walipaswa kuwalipa fidia Mashahidi hao watatu. Kwa kupendeza, Kamati hiyo ilisema kwamba “Mahakama ya Wilaya haikutaja sababu yoyote inayoonyesha kwamba wahusika hao wanapaswa kuandikishwa na Serikali ili waabudu pamoja kwenye nyumba ya kibinafsi.” Maneno hayo ni uthibitisho wa kwamba ndugu zetu nchini Azerbaijan wana haki ya kukutanika pamoja kwa ajili ya ibada bila kuandikishwa kisheria.

Kama ilivyokuwa katika kesi ya Rahima Huseynova, Kamati hiyo iliitaka Azerbaijan ipitie “sheria za chini, kanuni au utendaji” ili kuhakikisha kwamba wanatenda kulingana na haki zilizo katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).

Tunafurahi kwamba hali imebadilika Azerbaijan, na katika miaka ya hivi karibuni wenye mamlaka hawajavunja haki ya ndugu zetu ya kuabudu. Tunatumaini kwamba hukumu hizi mbili zitasaidia kazi ya kuhubiri habari njema nchini Azerbaijan isonge mbele.—Wafilipi 1:7.

a Novemba 2018, Mashahidi wa Yehova jijini Baku walisajiliwa kisheria na serikali ya Azerbaijan.