Hamia kwenye habari

Ndugu Royal Karimov na Ndugu Seymur Mammadov kutoka Azerbaijan

JANUARI 4, 2023
AZERBAIJAN

Ndugu Royal Karimov na Ndugu Seymur Mammadov Waachiliwa Huru Kutoka Kizuizini Nchini Azerbaijan

Ndugu Royal Karimov na Ndugu Seymur Mammadov Waachiliwa Huru Kutoka Kizuizini Nchini Azerbaijan

Ndugu Royal Karimov na Ndugu Seymur Mammadov wameachiliwa huru kutoka gerezani nchini Azerbaijan. Ndugu hao wawili walifungwa gerezani kwa kuwa walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Kama ilivyokuwa imeripotiwa awali, mahakama moja nchini Azerbaijan ilikataa ombi la Seymur la kufanya utumishi wa badala wa kiraia. Septemba 22, 2022, Seymur alihukumiwa kifungo cha miezi tisa gerezani. Hukumu hiyo ilikiuka maamuzi mawili yaliyotolewa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu dhidi ya Azerbaijan. Mawakili wa Seymur walikata rufaa lakini Desemba 12, 2022, Mahakama ya Rufaa ya Ganja ilibadilisha uamuzi huo ikasema hatafungwa gerezani lakini atapewa kifungo cha nje. Ingawa sasa Seymur yuko huru, amekata rufaa kwa Mahakama Kuu ya Azerbaijan ili ifutilie mbali uamuzi na kifungo hicho kisicho cha haki.

Seymur hakuruhusiwa kuwa na Biblia au kupokea barua alipokuwa gerezani lakini Yehova alimtegemeza. Anasema: “Siku moja kabla ya kesi yangu kusikilizwa mara ya mwisho mahakamani, niliandika maneno ya Yoshua 1:5, 6 kwenye kipande cha karatasi, andiko hilo linasema hivi: ’Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Musa. Sitakutupa wala kukuacha.’” Maneno hayo yalimwimarisha Seymur baada ya kukamatwa na kupelekwa gerezani. Anasema: “Nilisoma mistari hiyo miwili kila siku kama andiko la siku.”

Mei, 30, 2022, wenye mamlaka walimwagiza Royal afike kwenye Huduma ya Serikali ya Uhamasishaji na Usajili wa Eneo la Gadabay. Royal alikataa kuandikishwa jeshini kwa sababu ya dhamiri na akaomba apewe utumishi wa badala wa kiraia. Ombi lake lilikataliwa. Julai 25, 2022, maofisa wa jeshi walimkamata na kumweka kizuizini kinyume na sheria hadi Novemba 1, 2022. Royal ameomba matendo ya Huduma ya Serikali ya Uhamasishaji na Usajili wa Eneo la Gadabay yafanyiwe uchunguzi na walio na mamlaka ya kufanya hivyo.

Royal anasema hivi: “Nilipoambiwa kwamba sitaachiliwa, nilihisi vibaya sana, lakini nilijikumbusha kwamba hilo ni jaribu la imani.”

Royal alipokuwa kizuizini, dada yake aliruhusiwa kumtembelea na pia alifaulu kumpatia Biblia. Biblia hiyo ilimsaidia sana Royal kiroho. Anasema hivi: “Pindi fulani nilivunjika moyo lakini katika pindi hizo Yehova alinipa nguvu mpya. Nilipata amani isiyoelezeka niliposoma Biblia na kusali kwa Yehova.”

Tunaendelea kusali kwamba wenye mamlaka nchini Azerbaijan wataacha kuwafunga ndugu zetu gerezani wanapokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri, na tunatumaini pia kwamba wataandaa utumishi wa badala wa kiraia kama zinavyofanya nchi nyingine nyingi.​—1 Timotheo 2:1, 2.