Hamia kwenye habari

AGOSTI 24, 2018
AZERBAIJAN

Azerbaijan Yamhukumu Ndugu Yetu kwa Kukataa Utumishi wa Kijeshi

Azerbaijan Yamhukumu Ndugu Yetu kwa Kukataa Utumishi wa Kijeshi

Julai 6, 2018, Mahakama ya Wilaya ya Barda, Azerbaijan ilitoa hukumu yenye masharti ya mwaka mmoja kwa ndugu Emil Mehdiyev. Mahakama hiyo ilisema kwamba Emil mwenye umri wa miaka 18 alikuwa na hatia ya kukwepa utumishi wa kijeshi, lakini haikumfunga gerezani. Hata hivyo, hawezi kuhama bila kuwajulisha wenye mamlaka, na haruhusiwi kuondoka nchini Azerbaijan.

Mnamo Desemba 2017, Ndugu Mehdiyev alifika kwenye Kituo cha Kujiandikisha Jeshini cha Wilaya ya Barda. Alikataa kujiandikisha, kwa sababu dhamiri yake haikumruhusu kufanya utumishi wa kijeshi. Alipoagizwa afike kwenye kituo hicho, alienda ili kueleza msimamo wake unaotegemea dhamiri, na kuomba utumishi wa badala wa kiraia badala ya utumishi wa kijeshi. Aliambiwa kwamba hakukuwa na mpango kama huo na kwamba kesi yake ingewasilishwa kwenye ofisi ya mwendesha-mashtaka ya Wilaya ya Barda.

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa mara nyingi, Mahakama ya Wilaya ya Barda ilimhukumu kwa kutoa hukumu yenye masharti. Ingawa mahakama hiyo haikumfunga Emil gerezani, sasa anaonwa kuwa mhalifu na hakuna anachoweza kufanya ili kubadili jambo hilo kwa sababu serikali ya Azerbaijan haijaanzisha mpango wa utumishi wa badala wa kiraia, ingawa muda mrefu umepita tangu ilipoahidi kufanya hivyo.

Tunafurahi kwamba Ndugu Mehdiyev anadumisha msimamo wake wa kutounga mkono upande wowote licha ya kukabili hali hiyo ngumu.—1 Petro 2:19.