Hamia kwenye habari

Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova jijini Baku

DESEMBA 11, 2017
AZERBAIJAN

Mahakama ya Azerbaijan Yaamuru Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova Walipwe Fidia

Mahakama ya Azerbaijan Yaamuru Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova Walipwe Fidia

Agosti 4, 2017, mahakama ya wilaya jijini Baku, Azerbaijan, iliamuru kwamba Mashahidi wawili wa Yehova Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova walipwe fidia kutokana na madhara waliyopata kwa sababu ya kufungwa isivyo haki kwa miezi 11. Ingawa fidia hiyo ya pesa ni ndogo kwa kulinganisha na mateso waliyokabili, uamuzi huo umeonyesha wazi kwamba wenye mamlaka katika nchi hiyo waliwahukumu bila msingi wowote, jambo ambalo lilisababisha wapate madhara ya kihisia na kimwili, na likaharibu heshima yao kwa jamii.

Uamuzi Mzuri wa Mahakama Kuu Umeongoza kwenye Rufaa ya Kupata Fidia

Februari 8, 2017, Mahakama Kuu ya Azerbaijan ilifuta mashtaka ya uhalifu ya Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova waliyoshtakiwa kwa madai ya kusambaza machapisho ya kidini bila kibali cha nchi. Mahakama hiyo ilitambua kwamba broshua iliyotiliwa shaka ya Wafundishe Watoto Wako, ilikuwa imepata kibali cha kuingizwa nchini na haikuwa na madhara yoyote kwa jamii. Isitoshe, Mahakama ilitambua kwamba wanawake hao walikuwa na haki za msingi za kuwaeleza wengine kuhusu imani yao. Hukumu ya Mahakama Kuu ilitegemea haki zinazotolewa na Katiba ya Azerbaijan na mikataba ya kimataifa ambayo inatambuliwa na Azerbaijan.

Mahakama Kuu imeliacha suala la fidia mikononi mwa mahakama za kiraia. Wakati huohuo, Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova walipeleka malalamiko yao kwenye Mahakama ya Wilaya ya Nasimi Jijini Baku, wakitaka Wizara ya Fedha iwalipe fidia kutokana na mateso waliyokabili kutoka kwa Shirika la Usalama la Kitaifa (zamani idara hiyo iliitwa Wizara ya Usalama wa Taifa). Wanawake wote wawili walikuwepo mahakamani ingawa Bi. Zakharchenko alikuwa mgonjwa. Hakimu Shahin Abdullayev aliwaruhusu wasimulie kwa ufupi hali ngumu walizokabili.

Mahakama ya Wilaya Yakubali Kwamba Walitendewa Isivyo Haki

Uamuzi wa mahakama ya wilaya ulithibitisha tena azimio la Azerbaijan la kuheshimu haki za msingi za raia na wamezingatia kwa kiasi fulani malalamiko ya Mashahidi. Bi. Zakharchenko, ambaye afya yake imeathiriwa vibaya sana na hali ngumu za gerezani, atalipwa dola 5,737 za Marekani, na Bi. Jabrayilova ambaye ana umri mdogo akilinganishwa na Bi. Zakharchenko, atalipwa dola 4,828 za Marekani. Uamuzi ulisema hivi: “Mahakama inaamini kwamba walalamikaji walihukumiwa isivyo haki na kukamatwa kama wahalifu bila uthibitisho wa kosa, jambo lililofanya wapate madhara.”

Wizara ya Fedha ilikata rufaa kutokana na uamuzi uliotolewa kwamba Mashahidi hao wawili wapewe fidia. Novemba 20, 2017, Mahakama ya Rufaa ya Baku ilitupilia mbali rufaa ya Wizara hiyo na ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya wilaya.

Je, Maamuzi ya Mahakama Yatakuwa na Matokeo Mazuri?

Mashahidi wa Yehova wanavumilia hali ngumu wanapofanya utendaji wao wa kidini kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki zao za msingi za uhuru wa kuabudu na tishio la usalama wao. Wanaendelea kusumbuliwa, kutozwa faini, kutendewa isivyofaa wanapokutana ili kufanya ibada na wanaposhiriki katika utendaji wao wa kidini kwa amani. Serikali haijatoa utumishi wa badala wa kiraia kwa watu wanaokataa kujiunga na utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Wenye mamlaka wamekuwa wakikataa kuwasajili kisheria Mashahidi wa Yehova katika maeneo mengine nje ya jiji la Baku. Kwa sasa kuna malalamiko 18 yanayosubiri kusikilizwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na malalamiko 11 yamepelekwa kwenye Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu yanayohusu serikali kuwatendea vibaya Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan.

Mashahidi wa Yehova duniani kote wanatumaini kwamba maamuzi ya karibuni ya mahakama yatawachochea maofisa kuheshimu haki za waabudu wenzao nchini Azerbaijan.