MEI 8, 2018
AZERBAIJAN
Mahakama Kuu ya Azerbaijan Yaunga Mkono Fidia ya Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova
Aprili 16, 2018, Mahakama Kuu ya Azerbaijan iliunga mkono uamuzi wa mahakama ya chini wa kuwalipa fidia Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova kwa sababu ya kufungwa gerezani isivyo haki kwa miezi 11. Awali, mnamo Februari 2017, Mahakama Kuu iliwaachilia wanawake hao wawili walioshtakiwa kwa kusambaza machapisho ya kidini bila ruhusa ya Serikali. Hata hivyo, Mahakama Kuu iliacha suala la fidia lishughulikiwe na mahakama za kiraia.
Baada ya kufutwa kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili, Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, ambao ni Mashahidi wa Yehova, walianza kufuatilia fidia kupitia mahakama za kiraia ili walipwe kutokana na kutendewa vibaya. Agosti 2017, mahakama ya wilaya ilikubali wapewe fidia, lakini Wizara ya Fedha ikakata rufaa. Novemba 2017, mahakama ya rufaa iliunga mkono uamuzi wa mahakama ya wilaya. Kwa mara nyingine, Wizara hiyo ilipinga uamuzi huo na Februari 2018 ilifungua kesi kwenye Mahakama Kuu ili ipate ufafanuzi unaofaa wa sheria. Mahakama Kuu ilikataa rufaa ya Wizara na hivyo kuunga mkono uamuzi wa kwamba wanawake hao walipaswa kupewa fidia.
Zaidi ya kuwapa fidia, Mahakama Kuu ilitambua madhara waliyopata Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova walipokuwa wameshikiliwa na maofisa, ambao walitumia mamlaka yao vibaya na kukiuka haki za wanawake hao wasio na hatia.