Hamia kwenye habari

DESEMBA 13, 2016
AZERBAIJAN

Mashahidi wa Yehova Wakata Rufani Kupinga Faini Waliyotozwa kwa Kuwaambia Wengine Imani Yao

Mashahidi wa Yehova Wakata Rufani Kupinga Faini Waliyotozwa kwa Kuwaambia Wengine Imani Yao

Desemba 2, 2016, Polisi wa Kituo cha Wilaya cha Goranboy nchini Azerbaijan walimpeleka Ziyad Dadashov mahakamani kwa sababu ya utendaji wake wa kidini akiwa Shahidi wa Yehova. Wanaume wanne kutoka katika kijiji chake walithibitisha mahakamani kwamba Bw. Dadashov alizungumza kuhusu imani yake na kugawa machapisho ya Biblia. Hakimu Shirzad Huseynov wa Mahakama ya Wilaya ya Goranboy alimhukumu Bw. Dadashov kuwa na hatia ya kufanya utendaji wa kidini kinyume cha sheria a na akamtoza faini ya manat 1,500 (dola 846 za Marekani). Bw. Dadashov haamini kwamba anapaswa kuadhibiwa na hivyo atakata rufani kupinga uamuzi huo.

Katika eneo hilohilo, Jaarey Suleymanova na Gulnaz Israfilova walimtembelea mwanamke aliyekuwa akifurahia mazungumzo ya Biblia pamoja nao kwa miezi kadhaa. Kwa sababu hiyo, Polisi wa Kituo cha Wilaya cha Goranboy waliwashtaki wanawake hao wawili kwa kufanya utendaji wa kidini “nje ya eneo lililosajiliwa kisheria,” na Novemba 17, 2016, Hakimu Ismayil Abdurahmanli wa Mahakama ya Wilaya ya Goranboy aliwatoza wote wawili faini ya manat 2,000 (dola 1,128 za Marekani). Wanawake hao wamekata rufani kupinga faini hizo.

Jason Wise, mwanasheria wa kimataifa wa haki za kibinadamu, anasema hivi: “Ubaguzi dhidi ya Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan unaonyesha kwamba nchi hiyo haiheshimu Mkataba wa Ulaya. Mambo ambayo wenye mamlaka katika Wilaya ya Goranboy walifanya hayapatani kabisa na viwango vya uhuru wa ibada ambavyo nchi hiyo inadai kuzingatia.”

a Mashahidi wa Yehova wamesajiliwa kisheria jijini Baku, mji mkuu wa Azerbaijan. Bw. Dadashov alishtakiwa chini ya Sheria ya Kukiuka Mamlaka, Namba 515.0.4, “taasisi ya dini inayofanya kazi bila kusajiliwa kisheria.”