Hamia kwenye habari

MEI 26, 2014
AZERBAIJAN

Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan Wakata Rufani kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu

Mashahidi wa Yehova Nchini Azerbaijan Wakata Rufani kwa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu

Ilikuwa Jumapili asubuhi katika mkutano wa ibada. Takriban watu 200 kutia ndani wanaume, wanawake, na watoto walikuwa wamekusanyika katika chumba fulani jijini Baku, nchini Azerbaijan wakisikiliza hotuba ya Biblia.

Kisha ghafla polisi waliwavamia wakifuatiwa na maofisa wengine na wanahabari waliopiga picha tukio hilo. Polisi hao hawakuvuruga tu mkutano huo wa kidini wa Mashahidi wa Yehova bali pia waliwapiga wanaume kadhaa, wakafanya msako ndani ya nyumba hiyo bila idhini, wakawatukana wahudhuriaji, wakawanyang’anya pesa, kompyuta, na machapisho ya Biblia waliyokuwa nayo. Polisi hao waliwakamata wengi wa Mashahidi hao na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi na kuwazuilia kwa saa nyingi. Mashahidi sita kutoka nchi nyingine wanaohudumu nchini Azerbaijan walizuiliwa gerezani kwa siku kadhaa na kisha wakafukuzwa nchini humo. Vituo vya televisheni viliripoti tukio hilo kwa njia iliyowashushia heshima Mashahidi.

Matukio hayo ya Desemba 24, 2006 yalisababisha Mashahidi wa Yehova wawasilishe kwa mara ya kwanza malalamiko yao dhidi ya serikali ya Azerbaijan kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR). Tangu wakati huo, Mashahidi wamewasilisha malalamiko mengine 18 kwenye mahakama hiyo, malalamiko yanayohusu kukiukwa kwa haki ya kuwa na uhuru wa kidini.

MALALAMIKO

JUMLA

Kuvamiwa na Polisi

5

Kusajiliwa Upya

1

Kuishi Kupatana na Imani ya Kidini

2

Kukagua na Kuwekea Vizuizi Machapisho

5

Kufukuzwa Nchini

3

Kukataa Utumishi wa Kijeshi kwa Sababu ya Dhamiri

3

Jumla

19

Malalamiko yaliyowasilishwa kwenye mahakama ya ECHR dhidi ya serikali ya Azerbaijan, kufikia Januari 31, 2014

Mifano ifuatayo inaonyesha baadhi ya mambo ambayo Mashahidi wa Yehova nchini Azerbaijan wanakabili na ambayo yalisababisha waiombe msaada mahakama ya ECHR iwasaidie watendewe kwa haki.

  • Kunyimwa Fursa ya Kusajiliwa Upya

    Kikundi cha Kidini cha Mashahidi wa Yehova kilisajiliwa rasmi jijini Baku kwa mara ya kwanza Desemba 22, 1999, na kusajiliwa tena Februari 7, 2002 na Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Kazi na Mashirika ya Kidini (SCWRA). Mwaka wa 2009, serikali ya Azerbaijan ilirekebisha Sheria Kuhusu Uhuru wa Imani ya Kidini na ikataka mashirika yote ya kidini yasajiliwe upya. Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova liliwasilisha ombi lake la kutaka kusajiliwa, lakini SCWRA ikakataa ombi hilo kwa sababu ya kasoro fulani ndogo ya kisheria. Ingawa serikali haijafutilia mbali usajili uliofanyika mwaka wa 2002, imekataa kusajili upya Shirika la Kidini la Mashahidi wa Yehova kama inavyotakikana chini ya sheria yake mpya ya kusajili mashirika ya kidini.

  • Kusumbuliwa na Kunyanyaswa na Polisi

    Kila juma, Mashahidi wa Yehova hukutana faraghani kwenye nyumba za watu binafsi kwa ajili ya ibada. Mara kadhaa polisi wameingia kwa lazima kwenye nyumba hizo na kuvuruga ibada bila idhini ya kufanya hivyo. Wamewatendea wahudhuriaji kikatili, kuwazuilia kwa saa nyingi kwenye kituo cha polisi, na kuwanyang’anya machapisho ya kibinafsi wanayotumia kwa ajili ya ibada. Mashahidi wengine wametozwa faini kubwa. Mwaka wa 2011 Mashahidi sita kutoka Ganja walipatikana na hatia na wakatozwa faini ya takriban dola 12,000 za Marekani kwa kuhudhuria mkutano wa kidini ambao haukuwa umeidhinishwa na serikali. Siku za karibuni zaidi ambazo polisi wamevamia Mashahidi wa Yehova ni Januari 11 na Machi 2, 2014.

  • Kukagua na Kuwekea Vizuizi Machapisho

    Nchi ya Azerbaijan ndiyo nchi pekee iliyo katika Baraza la Ulaya a iliyoweka sheria ya kukagua na kuwekea vizuizi machapisho ya kidini, jambo linalokiuka katiba ya nchi hiyo. b Machapisho ya Biblia ambayo Mashahidi wanapokea kutoka nchi nyingine zilizo katika Baraza la Ulaya hukaguliwa na vizuizi kuwekwa kuhusiana na idadi itakayoruhusiwa nchini au nyakati nyingine yanapigwa marufuku. Miongoni mwa machapisho ambayo yamepigwa marufuku yanatia ndani matoleo kadhaa ya gazeti la Mnara wa Mlinzi ambalo ni chapisho la kidini la Mashahidi wa Yehova linalochapishwa mara mbili kwa mwezi. c Mahakama nchini Azerbaijan zimepuuza malalamishi ya Mashahidi yanayopinga vizuizi na marufuku iliyowekwa na Halmashauri ya Kitaifa Kuhusu Kazi na Mashirika ya Kidini.

Uchunguzi wa Jamii ya Kimataifa Kuhusu Jinsi Serikali ya Azerbaijan Inavyoshughulika na Mashirika ya Kidini

Mashirika kadhaa ya kimataifa yanayoshughulika na haki za kibinadamu yamefanya uchunguzi wao na yakatoa maoni kuhusiana na sheria ya mambo ya dini ya nchi ya Azerbaijan na jinsi nchi hiyo inavyoshughulika na mashirika ya kidini.

  • Ripoti ya mwaka wa 2013 inayotayarishwa kila mwaka na Tume ya Marekani Kuhusu Uhuru wa Kidini Kote Duniani inasema: “Licha ya madai ya nchi ya Azerbaijan kwamba inazingatia uhuru wa kidini na haki za kibinadamu za raia wake, uhuru wa kidini umezorota nchini humo, hasa baada ya kupitisha sheria inayodhibiti uhuru wa kidini ya mwaka wa 2009.”

  • Ripoti iliyotolewa na Tume ya Ulaya Inayopinga Ubaguzi wa Kidini na wa Kijamii (ECRI) ilishutumu sana hali ngumu zinazoathiri mashirika ya kidini. Kuhusu sheria ya nchi ya Azerbaijan ya uhuru wa ibada, tume hiyo ilisema hivi: “Tume ya ECRI inapendekeza kwa dhati kwamba serikali ya Azerbaijani ipatanishe sheria hiyo . . . na matakwa ya Mkataba wa Ulaya Kuhusu Haki za Kibinadamu.”

  • Tume ya Venice ya Baraza la Ulaya ilichapisha mapendekezo ya kina kuhusu mabadiliko ambayo nchi ya Azerbaijan inapaswa kufanya katika Sheria Kuhusu Uhuru wa Imani ya Kidini. Tume hiyo ilisema: “Sheria hiyo ina vipengele kadhaa ambavyo vinaenda kinyume na viwango vilivyopo vya kimataifa. . . . Baadhi ya mambo muhimu ya kisheria yanayohitaji kusuluhishwa ni kama vile upana wa sheria yenyewe na uhuru wa kidini na wa dhamiri wa wananchi, masuala ya usajili, masuala yanayohusu uhuru na vizuizi vya mashirika ya kidini; kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, suala la kuwashawishi watu wabadili imani yao, na kuchapisha na kusambaza machapisho ya kidini.”

Aina Mbalimbali za Uhuru Tunaothamini

Mashahidi wa Yehova duniani pote wanathamini sana uhuru wa kusema, kukusanyika, kushirikiana, na uhuru wa dhamiri na wa kidini. Wanathamini sana serikali zinazowaruhusu wafurahie haki hizo. Kikundi kidogo cha Mashahidi 2,500 nchini Azerbaijan pamoja na wale wote ambao hushirikiana nao katika ibada wanatumaini kwamba siku moja hata wao pia watafurahia uhuru mbalimbali wa kidini unaofurahiwa na dini nyinginezo nchini humo.

a Nchi ya Azerbaijan ilijiunga na Baraza la Ulaya Januari 25, 2001.

b Kifungu cha 48 kinatetea uhuru wa kidini nacho Kifungu cha 50 kinakataza kuwekea vizuizi au kupiga marufuku machapisho ya aina mbalimbali na vyombo vya habari.

c Kila mwezi Mashahidi wa Yehova huchapisha toleo la watu wote la gazeti la Mnara wa Mlinzi. Wanawaachia watu toleo hilo ili wajifunze yale ambayo Biblia inafundisha. Wanapokutana pamoja kila juma katika makutaniko yao, Mashahidi hujifunza Biblia kwa kutumia toleo la funzo la gazeti Mnara wa Mlinzi. Kila mwezi nakala 60,000,000 za Mnara wa Mlinzi hugawanywa katika lugha zaidi ya 200. Hakuna gazeti lingine duniani linalosambazwa kwa wingi jinsi hiyo.