Hamia kwenye habari

FEBRUARI 18, 2016
AZERBAIJAN

Nchi ya Azerbaijan Yawahukumu na Kuwaachilia Huru Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova

Nchi ya Azerbaijan Yawahukumu na Kuwaachilia Huru Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova

Huku wakiwa wamechoka na kudhoofika sana lakini wakiwa bila woga, Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Pirallahi jijini Baku mnamo Januari 28, 2016. Huku wakiwa wamefungiwa kizimbani kana kwamba ni wahalifu sugu, walimsikiliza Hakimu Akram Gahramanov alipokuwa akitoa hukumu. Hakimu huyo alitangaza kuwa wana hatia ya kugawa machapisho ya kidini bila kuwa na kibali cha Serikali na akamtoza kila mmoja wao faini ya manat 7,000 (dola 4,361 za Marekani). Kwa kuwa tayari walikuwa wametumikia kifungu cha gerezani kwa miezi 11, hakimu huyo alifuta faini hiyo na kuwaachilia huru.

Kifungo Kisichozingatia Haki

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Azerbaijan (MNS) ilidai kwamba Mashahidi wawili wa Yehova, Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, walifanya uhalifu kwa kumpatia jirani broshua inayotegemea Biblia bila malipo jijini Baku. Wizara hiyo ilifanya uchunguzi kwa majuma kumi kuhusiana na dai hilo na kuwahoji kwa ukali wanawake hao tena na tena. Walipokwenda kuisikiliza wizara hiyo ilipowaita Februari 17, 2015, walishangazwa waliposhtakiwa a na kufungwa gerezani.

Tangu mwanzo, wenye mamlaka waliwatendea wanawake hao kana kwamba ni wahalifu ambao ni “tishio kwa jamii.” Mmoja kati ya waliokuwa upande unaowatetea washtakiwa alisema hivi: “Nilishangazwa kusikia mpelelezi akihusisha matendo ya wanawake hao na maneno hayo ya ajabu. Alidai kwamba walikuwa na njama ya kufanya uhalifu na walivunja sheria kimakusudi. Ukweli ni kwamba Valida alirudi kuzungumza na mwanamke ambaye alikuwa amependezwa mapema na mazungumzo ya Biblia na alikuwa ameomba machapisho ya kidini. Mwanamke huyo aliwaalika Valida na Irina kwenye nyumba yake ili wapate chai na alichukua broshua ya kidini.”

Watendewa Kikatili na Kampeni Kubwa Yafanywa

Kizimbani

Kwa miezi 11 waliyokuwa gerezani, MNS iliwatenga Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova, kwa kuwakataza kutembelewa na wageni, kupigiwa simu, kutumiwa barua, au kuletewa Biblia. Maofisa wa MNS waliendelea kuwasababishia wanawake hao mkazo wa kiakili. Wanawake hao walikonda sana, hawakulala vya kutosha, na wakawa na afya mbaya. Mahakama ilikataa rufani zote zilizokatwa na maombi yote ya kuwapa kifungu cha nyumbani huku wakisubiri kusikilizwa kwa kesi yao.

MNS ilizidisha mateso yao kwa kuiomba mahakama iongeze muda wao wa kukaa gerezani kesi iliposikilizwa katika miezi ya Mei, Julai, na Septemba 2015. Hatimaye kesi iliposikilizwa mwezi wa Desemba, Hakimu Gahramanov aliahirisha kuisikiliza kesi hiyo mara tatu. Irina na Valida walikaa gerezani karibu mwaka mmoja kabla ya mahakama kutoa maamuzi yake Januari 28, 2016.

Uendeshaji wa kesi hiyo mahakamani ulibainisha kampeni kubwa ya MNS ya kuwapinga Mashahidi wa Yehova. MNS iliiomba mahakama iwafunge wanawake hao ili iwatafute Mashahidi wengine walioshiriki katika utendaji huo unaodaiwa kuwa wa kihalifu. Wanawake hao walipokuwa gerezani, maofisa waliwanyanyasa Mashahidi wa Yehova jijini Baku, wakiwahoji tena na tena na kuvamia nyumba zao na sehemu yao ya ibada.

Maombi ya Mataifa Mbalimbali ya Kuboreshwa kwa Hali

Mashahidi wa Yehova waliomba mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia haki za kibinadamu yawasaidie ili Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova waachiliwe huru . Walituma maombi kwenye Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu na katika mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa. Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote waliwatumia maofisa wa Azerbaijan maelfu ya barua. Wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova walizungumza na maofisa wa serikali katika nchi zao na kutuma barua moja kwa moja kwa rais wa Azerbaijan, wakimwomba aingilie kati jambo hilo.

Desemba 2, 2015, Kikundi cha Umoja wa Taifa Kinachoshughulikia Vifungo Vilivyo Kinyume cha Sheria (WGAD) kilieleza kwamba nchi ya Azerbaijan imekiuka haki za wanawake hao kwa jinsi ilivyowatendea na kuonyesha ubaguzi wa kidini. Kikundi hicho kiliwaambia maofisa wa Azerbaijan wawaachilie huru Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova na kuwalipa fidia kwa sababu ya kuwafunga kinyume cha sheria. Siku iliyofuata, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ya iliiomba serikali hiyo impe Bi. Zakharchenko kifungo cha nyumbani kwa sababu ya afya yake iliyokuwa inazidi kuzorota.

Mashtaka Yasiyo na Msingi ya Uhalifu

Wakati wa kusikiliza kesi, Hakimu Gahramanov alisikiliza maelezo kutoka kwa mwanamke anayedaiwa kutendewa uhalifu baada ya Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova kumpatia broshua. Hata hivyo, wakati wa kusikiliza kesi hiyo, mwanamke huyo alitoa ushahidi unaoleta utata na unapingana na maelezo yake ya mara ya kwanza. Alishindwa kueleza ni kwa jinsi gani aliathiriwa akiwa “aliyetendewa uhalifu” huo. Kisha hakimu akawapa nafasi Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova ya kumwuliza maswali mwanamke huyo. Wanawake hao walionyesha kwa heshima mambo yanayopingana na yasiyo sahihi katika ushahidi na maelezo ya mwanamke huyo. Wanawake wote wawili walimwambia “aliyedai kutendewa uhalifu” kwamba wamemsamehe.

Pia hakimu alisikiliza maelezo kutoka kwa “mashahidi” wawili kuhusu dai la kufanya uhalifu kwa kugawa machapisho ya kidini bila kuwa na kibali cha serikali. Mashahidi hao walitia sahihi maelezo yanayodai kwamba Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova wamefanya uhalifu, lakini walikiri kwamba hawakuwa wamesoma maelezo hayo. Walipoulizwa, walikiri kwamba hawawajui Irina na Valida na kwamba wanawake hao hawajawapa chapisho lolote la kidini. Maelezo ya shahidi wa tatu, yaliyosomwa kwa sauti na hakimu wakati wa kusikilizwa kwa kesi, yalikuwa yanapingana na yasiyo sahihi.

Licha ya ushahidi kuonyesha kwamba Bi. Zakharchenko na Bi. Jabrayilova hawakuwa na hatia, Hakimu Gahramanov alidai kuwa wana hatia kama walivyoshtakiwa. Baada ya kusikilizwa kwa kesi, wakili aliye upande unaotetea washtakiwa alisema hivi: “Niliona ni uamuzi wa kipumbavu. WGAD iliona jinsi wanawake hao walivyotendewa isivyo sawa na kuamuru waachiliwe huru na kulipwa fidia. Sasa, baada ya majuma mawili tu, hakimu anawapata na hatia wanawake hao.” Wanawake hao wanafuatilia haki zao kwa kukata rufani kwa sababu ya hukumu hiyo isiyo ya haki.

Azerbaijan Itaacha Lini Kuwatesa Mashahidi wa Yehova?

Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote, wanafarijika kujua kwamba Irina Zakharchenko na Valida Jabrayilova wako huru, wanahudumiwa na familia zao, na kupata matibabu yanayofaa. Mashahidi wanashangazwa kuona kwamba nchi ya Azerbaijan iliruhusu wanawake wawili wenye amani na wasio na hatia watendewe kikatili—na kuruhusu kitendo hicho kihalalishwe na mahakama.

Watu wengine wengi wanawaunga mkono Mashahidi kupinga ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa kidini unaofanywa na nchi ya Azerbaijan. Jumuiya ya kimataifa inatazama kwa makini kuona ikiwa serikali hiyo itaboresha jinsi inavyovitendea vikundi vidogo vya kidini. Mashahidi wa Yehova wanaendelea kutafuta fursa ili kuzungumzia mambo yanayoathiri ibada yao nchini Azerbaijan na kufikia mkataa na serikali.

a Katika hukumu yao iliyofanywa Novemba 10, 2015, mpelelezi wa MNS aliwashtaki wanawake hao kwa kuvunja Kifungu cha 167-2.2.1 cha Sheria ya Uhalifu ya Jamhuri ya Azerbaijan, inayokataza kikundi fulani kugawa machapisho ya kidini bila kuwa na kibali maalumu.