Hamia kwenye habari

FEBRUARI 4, 2020
BRAZILI

Usafi Unaendelea Kufanyika Baada ya Mafuriko Makubwa Kutokea Brazili

Usafi Unaendelea Kufanyika Baada ya Mafuriko Makubwa Kutokea Brazili

Tangu Januari 18, 2020, mvua kubwa sana imekuwa ikinyesha katika majiji ya Espírito Santo na Minas Gerais huko Brazili, na kusababisha mafuriko yaliyoleta madhara makubwa. Maji ya mafuriko yaliyokuwa yakipita barabarani yameharibu nyumba, yamesomba magari na kung’oa miti. Kulingana na taarifa za wenye mamlaka, maelfu ya watu walilazimika kuhama nyumba zao na watu zaidi ya 60 wamekufa.

Espírito Santo

Katika miji ya Iconha na Alfredo Chaves, mafuriko yameharibu nyumba tisa za Mashahidi wa Yehova, ambamo ndugu na dada 27 walikuwa wakiishi. Tunafurahi kwamba hakuna mwabudu mwenzetu hata mmoja aliyeumia au kufa.

Mashahidi karibu 100 kutoka katika eneo hilo wamejitolea kuwasaidia akina ndugu ambao wameathiriwa na mafuriko hayo. Chini ya mwongozo wa wazee, akina ndugu walitoa msaada wa chakula, maji, na nguo. Pia, walisaidia kusafisha na kuondoa matope kutoka ndani ya nyumba za ndugu zetu na za jirani zao.

Minas Gerais

Hakuna ndugu au dada yeyote aliyeumia au kufa. Hata hivyo, Majumba matano ya Ufalme yaliharibiwa na karibu familia 50 za Mashahidi zililazimika kuhama nyumba zao. Kwa sababu ya maji yaliyokuwa yakizidi kuongezeka, baadhi ya akina ndugu walikwama kwenye orofa ya pili katika nyumba zao na ilibidi waokolewe kwa kutumia mtumbwi. Wote waliolazimika kuhama nyumba zao, walienda kuishi katika nyumba za ndugu na dada wengine.

Halmashauri za Kutoa Msaada zimewekwa rasmi huko Espírito Santo na Minas Gerais ili kupanga kazi ya kutoa msaada katika majiji hayo. Halmashauri hizo zinafanya kazi pamoja na waangalizi wa mzunguko na wazee katika eneo hilo ili kushughulikia uhitaji wa kimwili na wa kiroho wa wahubiri walioathiriwa.

Tunaendelea kusali kwa ajili ya ndugu zetu walioathiriwa na mafuriko hayo. Tunamshukuru Yehova kwa kuwapa nguvu, faraja, na msaada wanaohitaji kupitia undugu wetu wa Kikristo.—Zaburi 28:7.