Hamia kwenye habari

Kushoto: Wageni wakikaribishwa kwenye banda la jw.org. Juu kulia: Dada ambaye ni kipofu na kiziwi akiwasiliana kwa kutumia lugha ya ishara kiganjani. Chini kulia: Sauti zilizorekodiwa za video zinazopatikana kwenye jw.org

OKTOBA 5, 2022
BRAZILI

Vipengele vya Walemavu vya JW.ORG Vyatangazwa Katika Maonyesho Nchini Brazili

Vipengele vya Walemavu vya JW.ORG Vyatangazwa Katika Maonyesho Nchini Brazili

Kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2022, Mashahidi wa Yehova walialikwa kushiriki kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Teknolojia (Reatech), yaliyofanyika jijini São Paulo, nchini Brazili. Reatech ni maonyesho ya kiteknolojia yanayojulikana sana katika Amerika ya Latini. Zaidi ya watu 46,000 walihudhuria maonyesho ya mwaka huu.

Katika maonyesho hayo kulikuwa na banda ambalo liliandaliwa na ndugu na dada zetu lililoonyesha tovuti yetu ya jw.org na programu ya JW Library na JW Library Sign Language. Vifaa vya kielektroni viliwekwa vilivyowawezesha watu kupata habari zaidi. Wahubiri ambao ni vipofu na wenye matatizo mengine ya kuona walikuwepo ili kuwaonyesha watu jinsi ya kutumia sehemu mbalimbali za tovuti yetu na programu hizo.

Mtaalamu mmoja anayewasaidia watu wenye ulemavu alipotembelea banda hilo alisema hivi: “Inavutia sana kuona kikundi cha kidini kinachojali sana na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.” Mtu mwingine alisema: “Hii ni njia yenye matokeo sana ya kuwasaidia walemavu kuwa sehemu ya jamii!”

Wawakilishi wa Shirika la Taifa la Vipofu Nchini Brazili (ONCB) walihudhuria maonyesho ya Reatech 2022. Walitangaza kwenye redio matukio yaliyokuwa yakiendelea katika maonyesho hayo. Siku ya kwanza na ya mwisho ya maonyesho hayo, akina ndugu waliofanya kazi kwenye banda letu walihojiwa kwenye redio. Walifafanua jinsi Mashahidi wa Yehova wanavyowasaidia vipofu, watu wenye matatizo ya kuona, na viziwi si tu nchini Brazili bali pia ulimwenguni pote. Wakati wa mahojiano hayo mwakilishi wa ONCB alisema kwamba jw.org ina video bora zaidi za lugha ya ishara ambazo amewahi kuona.

Ndugu wawili wakihojiwa na wawakilishi wa Shirika la Taifa la Viziwi Nchini Brazili

Tangu zamani hadi sasa, sikuzote Yehova amewaonyesha upendo watu wenye ulemavu. (Mambo ya Walawi 19:14) Tuna uhakika kwamba anafurahi sana anapoona Mashahidi wake wakiiga upendo wake. Tunatazamia kwa hamu wakati ambapo “macho ya vipofu yatafunguliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.”​—Isaya 35:5.