Hamia kwenye habari

DESEMBA 8, 2020
BULGARIA

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Uamuzi wa Kutetea Mashahidi wa Yehova Nchini Bulgaria

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Yatoa Uamuzi wa Kutetea Mashahidi wa Yehova Nchini Bulgaria

Novemba 10, 2020, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi kwamba serikali ya Bulgaria ilikuwa imeingilia uhuru wa ibada wa ndugu zetu. Uamuzi huo unamaanisha kwamba wenye mamlaka wanapaswa kuruhusu ujenzi wa Jumba la Ufalme katika jiji la Varna, Bulgaria uendelee. Mradi huo wa ujenzi umezuiwa kwa zaidi ya miaka kumi. Isitoshe, ECHR iliiamuru Bulgaria iwalipe ndugu zetu fidia ya euro 9,600 (dola 11,500 za Marekani).

Kesi hiyo ilihusu ujenzi wa Jumba la Ufalme katika eneo ambalo ndugu zetu walinunua Januari 2006. Wenye mamlaka wa jiji la Varna waliidhinisha ujenzi huo katika mwezi wa Mei 2007, na ndugu zetu wakaanza kazi mara moja. Lakini katika mwezi wa Julai mwaka huo, meya alisitisha ujenzi, akisema kwamba ndugu zetu walikiuka kanuni za ujenzi. Mwezi huo, chama cha kisiasa kinachojulikana sana nchini Bulgaria kiliweka mabango nje ya eneo la ujenzi na kufanya maandamano makubwa dhidi ya mradi huo wa ujenzi.

Kulingana na uamuzi wa ECHR, wenye mamlaka wa jiji la Varna walitoa tangazo la umma lililowashutumu Mashahidi wa Yehova na “kuunga mkono waziwazi maandamano hayo.” Pia, meya alipozungumza na vyombo vya habari alisema waziwazi kwamba anaunga mkono maandamano hayo.

Licha ya ubaguzi wa wazi, meya na maofisa wengine walidai kwamba walikuwa wakizuia ujenzi huo kwa sababu ya sheria zinazohusiana na ugawaji wa ardhi na si kwa sababu ya ubaguzi wa kidini.

Ndugu zetu walikata rufaa mara nyingi katika mahakama za Bulgaria, kutia ndani Mahakama Kuu, lakini hawakupata haki. Katika kipindi hicho, kutaniko la eneo hilo lililazimika kukodisha jumba la kufanyia mikutano.

ECHR ilisema kwamba matendo ya wenye mamlaka hao hayakuwa ya haki. Uamuzi ulioungwa mkono na mahakimu 6 kati ya 7 ulionyesha kwamba kwa kuzuia ujenzi wa Jumba hilo la Ufalme, wenye mamlaka wa jiji la Varna walikiuka “haki ya kuwa na uhuru wa fikira, dhamiri, na dini” iliyo katika Kifungu cha 9 na cha 11 cha Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu.

Ndugu zetu wanatumaini kwamba maofisa wa jiji la Varna watatekeleza kikamili uamuzi wa ECHR na kuwaruhusu wakamilishe ujenzi wa eneo lao la ibada kwa manufaa ya jamii na kwa utukufu wa jina la Yehova katika jiji hilo. Tunamshukuru Yehova kwa utegemezo wake.—Zaburi 54:4.