Hamia kwenye habari

Kuhubiri ujumbe wa Biblia kwa kutumia kigari cha machapisho jijini Sofia, Bulgaria

FEBRUARI 14, 2017
BULGARIA

Je, Mahakama za Bulgaria Zitatetea Uhuru wa Ibada?

Je, Mahakama za Bulgaria Zitatetea Uhuru wa Ibada?

Juni 4, 2016, Nikolai Stoyanov alikuwa amesimama kando ya kigari cha machapisho kwenye eneo la umma jijini Burgas, akiwapatia wapita njia machapisho ya Mashahidi wa Yehova bila malipo. Polisi walipofika kwenye eneo hilo saa 1:00 usiku, walimkamata na kumshtaki Nikolai kwa kukiuka sheria ya manispaa na wakamtoza faini ya leva 50 (sawa na dola 27 za Marekani). Nikolai alikuwa mmoja kati ya Mashahidi watano jijini Burgas walioshtakiwa na kutozwa faini katika miezi ya Mei na Juni kwa sababu ya utendaji wa dini wanaoufanya kwa amani.

Mahakama Zaamua Kwamba Halmashauri ya Jiji Ilipuuza Haki ya Uhuru wa Ibada

Nikolai na Mashahidi wengine wanne walikata rufaa kupinga hukumu na faini walizotozwa. Katika uamuzi wake uliofanywa Oktoba na Novemba 2016, Mahakama ya Mkoa ya Burgas ilithibitisha kwamba uhuru wa ibada wa Nikolai na Mashahidi wengine ulipuuzwa na hivyo faini walizotozwa zilifutwa.

Wakati huohuo, Mashahidi wa Yehova walitaka kujua ikiwa amri hiyo ya jijini Burgas ipo kwenye katiba. Oktoba 12, 2016, Mahakama ya Juu ya Burgas ilieleza kwamba sheria hiyo inayodaiwa kuzuia utendaji wa kidini wa Mashahidi inakiuka katiba ya Bulgaria na mikataba ya kimataifa ya uhuru wa ibada.

Halmashauri ya Jiji la Burgas tayari ilitambua kwamba vizuizi vilivyowekwa kwenye Sheria ya Kudumisha Amani Katika Jamii vinakiuka haki za kikatiba. Mwaka 2013, chama cha kisiasa cha nationalist kilikuwa kimetoa mapendekezo ya kurekebisha sheria hiyo, kikidai kwamba baadhi ya watu katika jamii walilalamika kuhusu utendaji wa kidini wa Mashahidi. Gavana wa wilaya hiyo alichunguza sheria hiyo na kufikia mkataa kwamba mapendekezo hayo yalionyesha ubaguzi na akatoa amri iliyosema kwamba sheria hiyo hafuati katiba. Hata hivyo, gavana aliyefuata alibatilisha amri hiyo na halmashauri ya jiji ikapitisha mapendekezo hayo ya marekebisho. Mchunguzi wa malalamiko ya wananchi aliionya halmashauri ya jiji kwamba maagizo hayo mapya yalipingana na sheria, lakini yaliendelea kutumiwa mpaka Mahakama ya Mkoa ya Burgas ilipoyabatilisha.

Hali kama hiyo imetokea Kyustendil, wakati halmashauri ya jiji ilikubali mapendekezo ya marekebisho kwa ajili ya sheria ya jiji ambayo inazuia uhuru wa ibada na kisha kuwaamuru polisi wa manispaa watekeleze mapendekezo hayo. Mahakama ya Juu ya Kyustendil ilibatilisha mashtaka sita ya uhalifu na faini za leva 800 hivi (sawa na dola 439 za Marekani) ambazo walitozwa Mashahidi kwa madai ya kufanya utendaji wa dini kinyume cha sheria, mahakama hiyo ilisema hivi kwenye mojawapo ya uamuzi wake: “Mtuhumiwa anawajibika kisheria kutokana kuwepo kwa sheria ambayo kihalisi inagusa mazoea yake yanayohusiana na haki yake ya uhuru wa ibada yanayoungwa mkono na Katiba pamoja na LRA [Sheria ya Utendaji wa Kidini].” Juni 24, 2016, mahakama hiyohiyo ilitoa hukumu iliyowaunga mkono Mashahidi na kusema kwamba mapendekezo hayo ya marekebisho yanapingana na katiba. a Halmashauri ya Jiji la Kyustendil imekata rufaa kwenye Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

Haki ya Kutangaza Imani ya Kidini Yapokewa Kwa Njia Tofauti-Tofauti

Miaka kadhaa iliyopita, manispaa 44 hivi nchini Bulgaria zilikuwa zimefanya marekebisho ya sheria ili kuzuia utendaji wa kidini wa taasisi za dini ambazo zimesajiliwa kisheria. Wenye mamlaka katika manispaa hizo wanapotekeleza sheria hizo, Mashahidi wamekabili maonyo, kuandikiwa ripoti mbaya, faini, vitisho, na hata kutendewa jeuri. Kwa mfano, Machi 26, 2016, Marin Tsvetkov, ofisa wa manispaa ya jiji la Vratsa, aliwatishia wanawake wawili ambao ni Mashahidi kwa kuwaambia kwamba angeleta kikundi cha vijana wahuni ili wawashambulie. Kisha akachukua na kuharibu baadhi ya machapisho yao ya kidini.

Hata hivyo, katika maeneo mengine ya Bulgaria, watu wanaokubali maoni ya wengine na mahakama zimetetea uhuru wa kidini. Juni 2, 2016, maofisa watatu walikifikia kikundi cha Mashahidi wa Yehova ambacho kilikuwa kikitumia kigari cha machapisho ili kuwahubiria watu kwenye jiji kuu la Sofia na kuwaomba vibali vya kufanya kazi hiyo ya kujitolea. Baada ya kuchunguza jambo hilo, maofisa hao walikubali kwamba Katiba ya Bulgaria inawapa haki Mashahidi hao kufanya utendaji huo wa amani. Katika jiji la Plovdiv, ambalo ndilo jiji la pili kwa ukubwa, halmashauri ya jiji hilo ilikataza vikundi vya kisiasa kutoa mapendekezo ya kurekebisha sheria ya Ulinzi na Usalama wa Jamii ili tu kuzuia utendaji wa dini ya Mashahidi wa Yehova.

Ni Nini Kitakachopata Sheria Hizo Zisizo Halali?

Mashahidi wa Yehova wamechukua hatua za kupinga uhalali wa sheria zote 44 ambazo kusudi lake ni kuzuia haki ya kikatiba ya kutangaza imani ya kidini. Krassimir Velev, msemaji wa ofisi ya kitaifa ya Mashahidi wa Yehova, iliyopo jijini Sofia, alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova wanafanya utumishi kwa jamii wanapozungumza na watu kuhusu mambo yanayowahangaisha na kuwapatia majibu yenye kuridhisha kutoka katika Biblia. Watu wengi wanakubali ujumbe wetu, lakini kwenye manispaa ambazo wamekubali sheria za kuzuia kazi yetu, tunashambuliwa tunapowapatia watu machapisho yetu bila malipo au tunapowaeleza imani yetu ya kidini hadharani. Inapohitajika tunalinda haki yetu yenye thamani tuliyopewa na Mungu ya uhuru wa ibada.”

Mashahidi wa Yehova wanafurahi kwamba maofisa wengi wenye vyeo vya juu na mahakama za Bulgaria zinatetea uhuru wa dini ambao ni jambo lenye manufaa kwa maeneo yote katika jamii. Wakati utaamua ikiwa wenye mamlaka watafanya marekebisho ya sheria nyingine zinazozuia utendaji wa kidini nchini Bulgaria.

a Bulgaria imetia sahihi Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu, ambao unatoa uhuru wa kidini au imani, katika ibada, mafundisho, mazoea, na kanuni za dini. Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (European Court of Human Rights) na Tume ya Ulaya inayohusu Demokrasia Kupitia Sheria (European Commission for Democracy Through Law) imeamua mara nyingi kwamba mkataba huo unawalinda Mashahidi wa Yehova wanapofanya kwa amani ibada zao au kuwahubiria majirani wao kuhusu imani yao.