Hamia kwenye habari

MEI 15, 2015
CHILE

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Chile

Mashahidi Watoa Msaada Baada ya Mafuriko Nchini Chile

Jumba la Ufalme jijini Copiapó lilijaa maji na matope.

SANTIAGO, Chile—Mvua kubwa ilinyesha eneo la Atacama kusini mwa Chile Machi 25, 2015, na kusababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko makubwa zaidi yaliyowahi kutokea kwenye eneo hilo katika miaka 80. Zaidi ya watu 30,000 wameathiriwa na msiba huo. Karibu watu 3,000 wamehamishiwa katika makao ya muda na 25 wamekufa.

Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Chile imeripoti kwamba hakuna Shahidi yeyote aliyekufa au kujeruhiwa vibaya. Hata hivyo, nyumba saba za Mashahidi zimebomolewa na nyingine nyingi kuharibiwa. Jumba moja la Ufalme, mahali pa ibada, lilibomoka na mengine mawili yaliharibiwa na mafuriko.

Mali iliyoharibiwa kwenye jiji la Diego de Almagro, ambalo liliathiriwa sana na mafuriko.

Katika jiji la Copiapó, moja ya majiji yaliyoathiriwa zaidi, Mashahidi wa Yehova walifanyiza kamati ya kutoa msaada ili kukusanya habari zinazohitajiwa na kupanga kazi ya usafi. Pia mwakilishi wa ofisi ya tawi ametumwa ili kuandaa msaada wa kiroho na kitia moyo kwa Mashahidi walioathiriwa. Mashahidi kutoka jiji la Antofagasta, Arica, Calama, Caldera, Iquique, na La Serena walituma misaada mara moja kwa ajili ya waabudu wenzao wenye uhitaji.

Mashahidi wakikusanya misaada kwenye Jumba la Ufalme katika jiji la Alto Hospicio ili ipelekwe kwenye maeneo yaliyoathiriwa.

Jason Reed, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Chile, alisema hivi: “Tunawasikitikia waathiriwa wa msiba huu, na kamati ya kutoa msaada imekusudia kuendeleza kazi ya kufanya usafi kwa muda mrefu na pia ya ukarabati. Tumeazimia pia kuandaa faraja na kitia moyo kwa kila mtu ambaye ameathiriwa na mafuriko.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Chile: Jason Reed, simu +56 2 2428 2600