Hamia kwenye habari

Mahakama ya Kikatiba ya Ekuado

SEPTEMBA 7, 2021
EKUADO

Mahakama ya Kikatiba ya Ekuado Imetetea Haki ya Uhuru wa Ibada ya Mashahidi wa Yehova

Mahakama ya Kikatiba ya Ekuado Imetetea Haki ya Uhuru wa Ibada ya Mashahidi wa Yehova

Agosti 24, 2021, Mashahidi wa Yehova walishinda kesi muhimu nchini Ekuado. Mahakama ya Kikatiba ilitangaza hukumu iliyosema kwamba haki ya uhuru wa ibada ilikuwa ikivunjwa katika jamii ya wenyeji wa asili wa San Juan de Ilumán katika Jimbo la Imbabura. Uamuzi huo wa Mahakama unasaidia kulinda haki ya uhuru wa ibada kwa ajili ya watu wote nchini Ekuado, hasa wale wanaoishi katika jamii za wenyeji wa asili, na kuweka msingi unaoweza kutumiwa katika nchi nyingine.

Mwaka wa 2014, viongozi wa jamii waliingia kwa nguvu katika eneo linalomilikiwa na Mashahidi wa Yehova na kuzuia ujenzi wa Jumba la Ufalme. Pia, waliwazuia ndugu na dada zetu wasikutane pamoja kwa ajili ya ibada na kuhubiri nyumba kwa nyumba. Ndugu zetu walifikisha jambo hilo mahakamani. Hata hivyo, mahakimu wawili wa eneo hilo waliotoa uamuzi dhidi ya Mashahidi wakidai kwamba haki zao za kikatiba hazikuwa zimekiukwa.

Baada ya kufanya yote wawezayo katika mahakama za chini ili kutatua hali hiyo, ndugu zetu walifikisha kesi hiyo kwenye Mahakama ya Kikatiba, mahakama kuu zaidi nchini humo. Mahakama ya Kikatiba ilitangaza kwamba mahakama za chini zilikiuka haki ya kisheria ya uhuru wa ibada. Viongozi wa jamii na mahakimu waliohusika waliamriwa wahudhurie masomo ambayo yatawasaidia kuelewa vizuri zaidi haki za kidini na za kitamaduni. Mbali na hilo, viongozi wa jamii hiyo waliombwa wasaidie “vikundi vya kidini na vilivyo na utamaduni mbalimbali kuishi pamoja kwa amani na hasa kulinda utendaji wa kidini” wa Mashahidi wa Yehova.

Philip Brumley, wakili mkuu wa Mashahidi wa Yehova alisema hivi: “Tunatambua kwamba haki za wenyeji wa asili ni ngao ya kulinda utamaduni wa asili, lakini isingefaa kugeuza ngao hiyo kuwa upanga unaodhuru haki za msingi za raia yeyote.”

Mashahidi wa Yehova huko San Juan de Ilumán wanashukuru kwa uamuzi huo wa Mahakama.

Tunashangilia kuona uthibitisho wa ‘mkono wa Yehova’ wakati ambapo ndugu na dada zetu wananufaika kutokana na ushindi wa kisheria unaolinda uhuru wetu wa ibada.—Methali 21:1.

Jumba la Ufalme la San Juan de Ilumá