Hamia kwenye habari

Ndugu Paulos Eyasu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam, ambao wamefungwa nchini Eritrea tangu Septemba 17, 1994

SEPTEMBA 17, 2019
ERITREA

Miaka 25 Kifungoni Nchini Eritrea

Miaka 25 Kifungoni Nchini Eritrea

Eritrea ndicho kitovu cha mojawapo ya mateso makali zaidi dhidi ya Mashahidi wa Yehova katika nyakati za kisasa. Kufikia Septemba 17, 2019, ndugu watatu, Paulos Eyasu, Isaac Mogos, na Negede Teklemariam, wamekuwa kifungoni kwa miaka 25. Isitoshe, kuna akina ndugu wengine 39 na dada 10 waliofungwa pia.

Hakuna ndugu au dada aliye kifungoni ambaye kufikia sasa amewahi kufikishwa mahakamani wala kuhukumiwa. Hawajui wataachiliwa lini. Akina ndugu wanne wamefia gerezani, na watatu walikufa baada ya kuachiliwa kwa sababu ya hali mbaya walizokabili.

Oktoba 25, 1994 ndipo mateso nchini Eritrea yalipoongezeka, karibu mwaka mmoja na nusu baada ya Eritrea kupata uhuru kutoka Ethiopia. Rais mpya alitangaza kwamba Mashahidi wa Yehova waliozaliwa Eritrea hawatambuliwi tena kuwa raia wa nchi hiyo hasa kwa sababu ya msimamo wao imara wa kutounga mkono upande wowote. Pia, rais huyo aliwanyima haki zao za msingi za kiraia. Aliwawekea Mashahidi wa Yehova vizuizi vingi kutia ndani kwamba hawawezi kupata elimu kamili, kumiliki biashara, au kusafiri nje ya nchi.

Katika miaka ya karibuni, mashirika ya haki za kibinadamu yanayofahamika yameonyesha kwamba yanahangaishwa sana na jinsi Eritrea imepuuza viwango vya haki za kibinadamu vya kimataifa, hata katika kesi zinazowahusu Mashahidi wenzetu. Eritrea imekataa kufuata mapendekezo yaliyotolewa na mashirika hayo.

Ona: “RIPOTI YA PEKEE: Mateso ya Mashahidi wa Yehova Nchini Eritrea

Tutaendelea kuwafahamisha maofisa wa serikali na wengine wenye mamlaka kuhusu hali iliyopo nchini Eritrea. Ndugu na dada zetu wanapoendelea kuonyesha imani na ujasiri licha ya mateso wanayokabili, tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kuwa Msaidizi na ‘mwamba wanaoukimbilia.’—Zaburi 94:22.