Hamia kwenye habari

OKTOBA 14, 2014
GEORGIA

Georgia Yashinikizwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Kutekeleza Sheria

Georgia Yashinikizwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu Kutekeleza Sheria

Oktoba 7, 2014, Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) ilitoa uamuzi uliowatetea Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Georgia. Kesi hiyo, Begheluri na Wengine dhidi ya Georgia, inayohusisha watu 99 katika visa 30 vya kupigwa na kutukanwa ilipelekwa mahakamani miaka zaidi ya 12 iliyopita. Wote wanaohusika ni Mashahidi wa Yehova isipokuwa mmoja. Visa hivyo vilianza polisi wengi walipovuruga makusanyiko mengi ya kidini na hatimaye fujo hizo za chuki ya kidini zikaenea hadi kwenye nyumba za Mashahidi, mahakamani, na mitaani.

Uamuzi wa ECHR ulitaja kwamba walalamishi walipeleka malalamishi yapatayo 160 kwenye ofisi za mamlaka za upelelezi, na walalamishi hao walidai kuwa polisi na maofisa wengine wa serikali walihusika moja kwa moja katika baadhi ya mashambulizi hayo. Hata hivyo, malalamishi hayo hayakufuatiliwa kikamili. Kwa kuwa wahusika hawakuadhibiwa, walipata ujasiri wa kuendelea na mashambulizi zaidi.

Septemba 8, 2000, kusanyiko la kidini la Mashahidi wa Yehova lavamiwa

Kwa mfano, Septemba 8, 2000, Mashahidi 700 hivi walikusanyika kwa ajili ya ibada katika jiji la Zugdidi. Kwa ghafla, polisi wa kikosi maalumu (SWAT) waliofunika nyuso walivamia eneo hilo la kusanyiko, wakaliteketeza jukwaa, na kuwapiga watu karibu 50 waliokuwa wakiabudu. Waathiriwa walipeleka malalamishi upesi kwa wenye mamlaka. Hata hivyo, wenye mamlaka walikataa kuwashtaki wahusika, na waliodhulumiwa wakaachwa bila msaada wowote wa kisheria.

ECHR Yashutumu Mamlaka kwa Kutochukua Hatua Zifaazo

Kwa sababu mamlaka za kutekeleza sheria zilishindwa kufanya uchunguzi haraka na kuwaadhibu waliohusika, waathiriwa waliungana na kupeleka malalamishi yao kwenye mahakama ya ECHR mwaka wa 2002. Katika uamuzi uliofanywa Oktoba 7, mahakama ya ECHR ilisema kwamba “mamlaka za Georgia zimechangia kuongezeka kwa uhalifu, na zimechochea kuvamiwa kwa Mashahidi wa Yehova kotekote nchini humo.” Mahakama hiyo ilisema pia kwamba mashambulizi hayo ya jeuri “yalichochewa na chuki kali isiyo na msingi dhidi ya Mashahidi wa Yehova” na kwamba mamlaka za kutekeleza sheria zilionyesha “mtazamo kama huo wa ubaguzi . . . , uliothibisha kwamba mamlaka hizo zilitelekeza jeuri hiyo.”

“Mamlaka za Georgia zimechangia kuongezeka kwa uhalifu, na zimechochea kuvamiwa kwa Mashahidi wa Yehova kotekote nchini humo.”

Begheluri na Wengine dhidi ya Georgia, na. 28490/02, 7 Oktoba 2014, p. 40, fu. 145

Kwa sababu hiyo, mahakama ya ECHR iliamua kwamba mamlaka za Georgia zina hatia ya kuwatendea bila huruma walalamishi 47 na kwamba ziliwabagua walalamishi 88 na kuwanyima uhuru wao wa kidini. ECHR iliiamuru serikali ya Georgia “kukomesha uvunjaji huo wa sheria na kurekebisha tatizo hilo” la kutochukua hatua na kuondoa “chuki kali isiyo na msingi.” ECHR iliiamuru serikali ya Georgia kuwalipa walalamishi faini ya Euro zaidi ya 45,000 kwa kuwadhulumu na kugharimia kesi hiyo.

Hali ya Mashahidi Nchini Georgia Yaboreshwa

Ingawa hali zimekuwa bora zaidi tangu 2004, Mashahidi nchini Georgia bado wanaendelea kuvamiwa na kudhulumiwa mara kwa mara. Mwaka wa 2013, kuliripotiwa visa 53 vya kushambuliwa kwa Mashahidi. Uamuzi katika kesi ya Begheluri unazishurutisha mamlaka za Georgia kufanya uchunguzi haraka na kuchukua hatua zifaazo dhidi ya uhalifu uliotekelezwa dhidi ya raia wa nchi hiyo. Mashahidi wa Yehova wanatarajia kwamba serikali itawashtaki na kuwaadhibu, bila ubaguzi wowote, wahusika walio na hatia ya uhalifu unaochochewa na chuki ya kidini.