Hamia kwenye habari

APRILI 15, 2015
GEORGIA

Mashahidi wa Yehova Wazindua Kampeni ya Pekee Mwezi wa Aprili

Mashahidi wa Yehova Wazindua Kampeni ya Pekee Mwezi wa Aprili

Aprili 1, 2015, Mashahidi wa Yehova walizindua kampeni ya kujulisha idara zote za polisi, halmashauri za miji, na ofisi za waendesha-mashtaka kotekote katika Jamhuri ya Georgia kuhusu uamuzi muhimu wa karibuni. Uamuzi huo uliopitishwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) katika kesi ya Begheluri and Others v. Georgia, ulihusu ukiukwaji wa haki za Mashahidi wa Yehova nchini Georgia. Kampeni ilitoa habari hususa kuhusu kesi hiyo, uamuzi uliofikiwa, na utendaji wa kidini wa Mashahidi wa Yehova kwa mamlaka husika.

Historia ya Georgia ya Kuruhusu Vitendo vya Jeuri

Kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2003, wafuasi wa mwanamume aliyeachishwa ukasisi katika kanisa la Othodoksi waliwashambulia vikali Mashahidi wa Yehova. Ingawa Mashahidi waliwasilisha malalamiko 784 ya visa hivyo na vingine kama hivyo kwa polisi, wenye mamlaka waliyapuuza au walijihusisha katika visa hivyo dhidi ya Mashahidi. Hakuna hata moja kati ya malalamiko hayo ya Mashahidi yaliyozaa matunda. Kutochukua hatua kwa mamlaka za Georgia, kuliwapa ujasiri wenye kufanya vitendo hivyo vya jeuri, hata wamewashambulia Mashahidi ndani ya mahakama, katika makusanyiko makubwa ya kidini, na barabarani.

ECHR Yatoa Uamuzi Muhimu

Mashahidi wa Yehova nchini Georgia waliwasilisha kesi mbili kwenye ECHR ili kutatua tatizo hilo. Mahakama ilitoa hukumu ya kesi ya kwanza Mei 2007, a na kesi ya pili—Begheluri and Others v. Georgia—Oktoba 2014. Katika hukumu hizo mbili, ECHR iliishutumu serikali ya Georgia kwa kuhusika katika mashambulizi hayo, ikionyesha wazi uhusiano kati ya serikali kutochukua hatua na kuongezeka kwa jeuri. ECHR ilieleza hivi katika uamuzi wa kesi ya Begheluri; “mamlaka za Georgia ni kana kwamba zimeruhusu uvunjaji wa sheria kwa kutochukua hatua, jambo lililochochea mashambulizi zaidi dhidi ya Mashahidi wa Yehova kotekote nchini.” b

Kwa kupendeza, siku iliyofuata, baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kesi ya Begheluri, serikali ya Georgia ilitoa taarifa rasmi, ikiapa kuzuia visa vingine vya jeuri:

“Georgia imeazimia kulinda uhuru wa kufikiri, dhamiri, na wa kidini kutia ndani haki za kibinadamu kwa ujumla. Nchi hiyo imeazimia kuhakikisha kuna usawa mbele ya sheria na kuwatoza hesabu wakiukaji wa haki za kibinadamu. Kihususa, haitaruhusu tena uvunjaji wa sheria au kuvumilia vitendo vya jeuri.”

Mabadiliko Mazuri Nchini Georgia

Mashahidi wa Yehova nchini Georgia leo wana hali tofauti kabisa ikilinganishwa na miaka iliyopita. Wanafanya ibada kwa amani na wanathamini kwamba sasa wenye mamlaka kwa ujumla wanatetea haki zao. Mashahidi wa Yehova wamejenga nyumba za ibada na kupanua ofisi yao ya tawi.

Hata hivyo, baadhi ya wenye mamlaka hawajui mengi kuhusu Mashahidi wa Yehova au imani yao na huenda hawajui lolote kuhusu uamuzi wa kesi ya Begheluri au hiyo taarifa rasmi ya serikali. Bado vitendo vya jeuri vinavyochochewa na ubaguzi wa kidini hufanyika bila hatua kuchukuliwa—kwa mfano, katika mwaka wa 2014, Mashahidi walitendewa kwa jeuri katika visa 30. Mashahidi wa Yehova wamewasilisha kesi nyingine tena kwenye ECHR kutatua tatizo hilo. c

Kampeni hiyo ya mwezi wa Aprili itasaidia kuboresha haki za kibinadamu kotekote nchini Georgia. Mashahidi wa Yehova wanaishukuru serikali ya Georgia kwa msimamo wake wa kutoruhusu tena uvunjaji wa sheria, na wanatarajia serikali iendelee kuwa thabiti katika kuwachukulia hatua watu wenye hatia ya kufanya vitendo vya uhalifu kwa sababu ya chuki ya kidini.

a Members of the Gldani Congregation of Jehovah’s Witnesses and Others v. Georgia, na. 71156/01, 3 Mei 2007.

b Begheluri and Others v. Georgia, na. 28490/02, § 145, 7 Oktoba 2014.

c Tsartsidze v. Georgia, na. 18766/04, kesi iliwasilishwa 26 Mei 2004 — Walioshambuliwa na mamlaka za serikali au kushambuliwa wenye mamlaka wakishuhudia; Biblaia and Others v. Georgia, na. 37276/05, kesi iliwasilishwa 10 Septemba 2005 — Walioshambuliwa na mamlaka za serikali au kushambuliwa wenye mamlakawakishuhudia; Tsulukidze and Others v. Georgia, na. 14797/11, kesi iliwasilishwa 27 Januari 2011 — Kutofanya uchunguzi kamili na kutowashtaki waliohusika katika mashambulizi tisa yaliyochochewa na ubaguzi wa kidini.