Hamia kwenye habari

Mashahidi watatu wa Georgia waliovaa mavazi ya asili wakipiga picha na wajumbe wawili kusanyikonin.

NOVEMBA 22, 2018
GEORGIA

Kusanyiko la Kwanza la Pekee Kufanywa Tbilisi, Georgia

Kusanyiko la Kwanza la Pekee Kufanywa Tbilisi, Georgia

Ndugu na dada nchini Georgia waliwakaribisha wahudhuriaji kutoka nchi 18 kwenye Kusanyiko la Pekee la “Uwe Jasiri”! lililofanywa kwenye mji mkuu, Tbilisi, Julai 20-22, 2018. Tukio hilo la kitheokrasi, ambalo limefanywa kwa mara ya kwanza nchini Georgia, lilihusisha karamu kubwa ya kiroho, ukarimu, na pindi za kufurahia utamaduni na historia ya eneo hilo.

Kusanyiko hilo lilifanywa kwenye uwanja ulioko Tbilisi unaoitwa Olympic Palace, na lilikuwa na kilele cha wahudhuriaji 7,002. Programu ilirushwa katika maeneo mengine 80 hivi nchini kote, hivyo, kwa ujumla hudhurio lilikuwa watu zaidi ya 21,500. Jambo moja la kupendeza sana ni ubatizo wa ndugu na dada wapya 208.

Zaidi ya programu ya kiroho, wajumbe walifurahia utamaduni wa Kigeorgia. Mashahidi wenyeji waliwatumbuiza wageni kwa dansi na muziki, chakula cha kitamaduni, na matembezi kwenye jiji la kale la Tbilisi.

Tamaz Khutsishvili, mwakilishi wa ofisi ya tawi nchini Georgia, alisema hivi: “Uhuru wa kidini haujakuwepo muda wote. Lakini katika kisa hiki, wenye mamlaka wameshirikiana nasi na tumekuwa na tukio lisilosahaulika la kuwakaribisha ndugu wengi kufurahia [kusanyiko la pekee] pamoja nasi.”—Waroma 15:7.

 

Kulikuwa na kilele cha wahudhuriaji 7,002 kwenye kusanyiko la pekee katika uwanja wa Olympic Palace Julai 20-22, 2018. Watu wengine 14,912 walifurahia kuona programu hiyo ambayo ilipeperushwa kotekote nchini.

Ndugu Stephen Lett, mshiriki wa Baraza Linaloongoza, alitoa hotuba ya mwisho kila siku kusanyikoni.

Jambo moja la kupendeza sana ni ubatizo wa ndugu na dada 208. Kidimbwi cha ubatizo kilikuwa karibu na mwamba ulio sehemu ya ndani ya uwanja wa Olympic Palace.

Video ya kusanyiko ilipeperushwa kwenye maeneo 80 hivi.

Dada nchini Georgia wakimkaribisha mjumbe kutoka taifa lingine. Dada mmoja amevaa kofia iliyotengenezwa kutokana na manyoya ya kondoo ambayo kwa kawaida inavaliwa na watu wengi wanaoishi maeneo ya milimani ya Georgia.

Programu ya kupendeza ilipangwa Julai 17 na 18 kwenye eneo la Château Mukhrani, lililo katika kijiji cha Mukhrani, karibu na Tbilisi. Programu ilihusisha muziki wa kitamaduni wa Georgia, dansi, na video mbili zilizosimulia historia ya kitheokrasi nchini Georgia.

Mashahidi wenyeji wakicheza dansi ya Adjaruli (jina linalotokana na Adjara, eneo lililo kusini-magharibi ya nchi hiyo, karibu na Bahari Nyeusi). Dansi hiyo inapendeza hata zaidi kwa sababu ya nguo za kitamaduni za eneo hilo zenye rangi nyangavu.

Ndugu wakiimba wimbo wa kitamaduni katika mtindo uliotumiwa kale nchini Georgia.