OKTOBA 20, 2015
GHANA
Mashahidi Nchini Ghana Watoa Msaada Mara Moja Baada ya Mafuriko
ACCRA, Ghana—Mwishoni mwa mwezi Agosti 2015, Mashahidi wa Yehova walimalizia kutoa msaada katika mji mkuu wa Ghana, Accra, uliokumbwa na mafuriko makubwa yaliyoharibu nyumba na kuua watu zaidi ya 200.
Ingawa hakuna Mashahidi waliokufa, nyumba za Mashahidi 250 hivi ziliharibiwa na mafuriko. Juni 4, 2015, siku moja baada ya mafuriko kutokea, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Ghana ilianzisha halmashauri ya kutoa msaada ili kuhakikisha kwamba waathiriwa wa mafuriko wanapata blanketi, nguo, na maji. Halmashauri hiyo ilifanya mipango ili kusafisha na kurekebisha nyumba zilizoharibiwa na mafuriko. Mashahidi katika jiji la Accra ambao nyumba zao hazikuharibiwa na mafuriko waliwakaribisha na kuishi na waabudu wenzao ambao nyumba zao ziliharibiwa.
Mafuriko yalisababisha mlipuko katika kituo cha mafuta ya petroli ambao uliharibu mabomba ya maji katika eneo la Adabraka na kusababisha eneo lote kukosa maji. Ofisi ya tawi ilinunua tangi la maji na kuliweka katika Jumba la Ufalme (nyumba ya ibada) la Adabraka kwa ajili ya Mashahidi na majirani zao.
Jumamosi, Juni 6, ofisi ya tawi ilituma vikundi viwili vya wataalamu wa afya, vilivyokuwa na jumla ya madaktari watano na wauguzi wawili, ambao wote ni Mashahidi, ili kuwahudumia waabudu wenzao na waathiriwa wengine wa mafuriko katika maeneo ya Alajo na Adabraka. Walitibu magonjwa mbalimbali kama vile malaria, magonjwa ya kifua, na kuhara. Wawakilishi wa ofisi ya tawi na Mashahidi walio karibu na eneo hilo waliwatembelea pia waabudu wenzao ili kuwafariji kiroho na kihisia.
Msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Ghana, Nathaniel Gbedemah, anasema hivi: “Tunasikitika sana kutokana na uharibifu na vifo vilivyosababishwa na mafuriko yaliyoikumba Accra. Kama ambavyo Mashahidi wa Yehova katika nchi nyingine wanavyofanya, sisi pia tunafanya yote tuwezayo ili kutoa msaada wa kihisia, kimwili, na kiroho kwa ajili ya watu wote walioathiriwa na janga hili.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000
Ghana: Nathaniel Gbedemah, simu +233 30 701 0110