Hamia kwenye habari

JUNI 16, 2016
HAITI

Serikali ya Haiti Yawapa Tuzo Mashahidi kwa Kuwasaidia Walemavu

Serikali ya Haiti Yawapa Tuzo Mashahidi kwa Kuwasaidia Walemavu

PORT-AU-PRINCE, Haiti—Ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani inayowasaidia walemavu nchini Haiti (BSEIPH) ilitoa tuzo kwa shirika la kisheria la Mashahidi liitwalo Christian Association of Jehovah’s Witnesses in Haiti. Ofisi hiyo hutambua mashirika yanayowasaidia walemavu. Msemaji wa Mashahidi wa Yehova Daniel Lainé alipokea tuzo ya “Mawasiliano na Teknolojia” katika sherehe iliyohudhuriwa na waziri mkuu Evans Paul, kama picha inavyoonyesha. Tukio hilo lilifanyika Desemba 3, 2015, Siku ya Walemavu.

Tuzo ambayo Mashahidi walipokea ya “Mawasiliano na Teknolojia” kwa kuwasaidia walemavu, Desemba 3, 2015.

Akizungumzia jinsi Mashahidi wanavyowasaidia walemavu, Guerline Dardignac, katibu wa BSEIPH, alisema kwamba “shirika la Christian Association of Jehovah’s Witnesses in Haiti limefanya jitihada za pekee kuwahusisha walemavu katika shughuli mbalimbali. Shirika hilo huhakikisha kwamba majengo yao yanaweza kutosheleza mahitaji ya walemavu; pia shirika hilo huhakikisha kwamba wanaweza kuwasiliana na pia kutumia teknolojia kwa kuendesha mikutano ya ibada na shughuli nyingine katika lugha ya ishara (Lugha ya Ishara ya Marekani) na kuwapatia watu machapisho yenye maandishi ya vipofu na video za lugha ya ishara.”

Mwaka wa 2013, Mashahidi walipokea tuzo ya kuwasaidia walemavu kwa sababu ya jitihada zao za kufanya jengo lao la ibada liweze kutumiwa na walemavu huko Cayes, Haiti.

Hii ni tuzo ya pili ambayo Mashahidi wamepewa kwa kuwasaidia walemavu tangu tetemeko kubwa la ardhi lilipotokea nchini Haiti. Tetemeko hilo liliwaua watu zaidi ya 222,000 na kuwajeruhi watu 300,000 hivi, jambo ambalo liliongeza idadi ya walemavu kwa asilimia 15 hivi. Walipokea tuzo ya kwanza mwaka wa 2013 wakati BSEIPH ilipotambua jitihada za Mashahidi za kufanya jengo lao la ibada liweze kutumiwa na walemavu huko Cayes, Haiti.

Bw. Lainé alisema hivi: “Tunashukuru sana kwa tuzo hizi zinazoonyesha kutambuliwa kwa jitihada zetu za kuwasaidia walemavu, na tunafurahi kutoa huduma hizo kwa sababu ni sehemu ya kazi yetu ya elimu ya Biblia.”

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, 1-718-560-5000

Haiti: Daniel Lainé, 509-2813-1560