Hamia kwenye habari

Jengo la Palacio de las Cortes jijini Madrid, Hispania, ambapo Bunge hukutana

MEI 24, 2023
HISPANIA

Hispania Imewapa Mashahidi wa Yehova Msamaha wa Kodi

Hispania Imewapa Mashahidi wa Yehova Msamaha wa Kodi

Aprili 26, 2023, serikali ya Hispania iliidhinisha mabadiliko makubwa katika sheria ya kodi nchini humo. Uamuzi huo unawaathiri Mashahidi wa Yehova nchini Hispania katika njia kadhaa zinazofaa.

Uamuzi huo wa serikali umetoa msamaha wa kodi ya majengo yote ya kitheokrasi ya tengenezo letu nchini humo. Pia uamuzi huo unawaruhusu watu mmojammoja nchini Hispania kupata punguzo la tozo kwa michango wanayotoa kwa ajili ya kazi ya Mashahidi wa Yehova. Isitoshe, badiliko hilo linathibitisha kwamba Mashahidi wa Yehova ni “dini inayotambuliwa” kama inavyothibitishwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

Ndugu Joan Comas (kushota), mwakilishi wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Hispania, akiwa na Bw. Félix Bolaños (kulia), kutoka kwenye Ofisi ya Rais

Ingawa Juni 2006 Mashahidi wa Yehova nchini Hispania walitambuliwa kisheria kuwa dini inayotambuliwa, Mashahidi hawakupewa msamaha wa kodi kama dini nyingine zote nchini humo. Ndugu zetu waliendelea kujaza maombi ya kupata msamaha huo. Bila kutarajiwa, Aprili 24, 2023, maofisa katika Ofisi ya Rais waliwakaribisha wawakilishi wa Mashahidi wa Yehova nchini Hispania kwenye mkutano. Kwenye mkutano huo, ndugu zetu walijulishwa kwamba sheria kuhusu kodi ya mashirika yasiyo ya kibiashara ilikuwa ikibadilishwa, na hilo lingetia ndani Mashahidi wa Yehova. Siku mbili baadaye, Aprili 26, 2023 Bunge liliidhinisha marekebisho hayo ya sheria. Inatarajiwa kwamba mabadiliko hayo katika sheria yataanza kutumika rasmi mnamo Juni 2023.

Tunafurahi sana kupata uamuzi huo muhimu unaothibitisha zaidi uhuru wa ibada wa Mashahidi wa Yehova nchini Hispania.​—Wafilipi 1:7.