AGOSTI 16, 2019
INDIA
Mafuriko Yaikumba India Magharibi
Kulingana na vyombo vya habari, mafuriko yaliyotokea magharibi mwa India yamewaua watu wapatao 169 katika miji ya Gujarat, Maharashtra, Karnataka, na Kerala.
Ofisi ya tawi ya India imeripoti kwamba hakuna ndugu au dada aliyekufa au kujeruhiwa katika mafuriko hayo. Ofisi ya tawi imetoa habari zifuatazo.
Gujarat: Katika jiji la Vadodara, wahubiri wapatao 145 waliathiriwa na mafuriko hayo. Ofisi ya utafsiri ya Gujarati iliyoko Vadodara, haikuathiriwa na mafuriko.
Maharashtra: Huko Mumbai, nyumba za familia sita ziliharibiwa. Katika jiji la Sangli, lililo kilomita 378 kusini mashariki mwa Mumbai, wahubiri 25 walilazimika kuhama nyumba zao. Akina ndugu wanaoishi katika jiji la karibu waliwapa makazi ya muda.
Karnataka: Familia sita zililazimika kuhama nyumba zao kwa sababu ya mafuriko. Ofisi ya tawi iko katika jiji hili lakini haikuathiriwa na mvua hizo kubwa zilizosababisha mafuriko.
Kerala: Familia zipatazo 100 zimehamia maeneo yaliyo juu na kwa sasa wanaishi na Mashahidi wengine. Halmashauri ya Kutoa Misaada inachunguza jinsi hali ilivyo.
Ofisi ya tawi inasimamia shughuli za kutoa misaada katika maeneo yaliyoathiriwa. Waangalizi wa mzunguko na akina ndugu wanaofanya kazi katika Idara ya Usanifu Majengo na Ujenzi wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii ili kutathmini na kusaidia ndugu na dada walioathiriwa. Hilo linatia ndani kutoa misaada ya mahitaji ya msingi ya vitu vya kimwili, kama vile maji ya chupa na kitia moyo cha kiroho.
Tunasali kwamba Yehova aendelee kuwa pamoja na ndugu zetu walioathiriwa na mafuriko hayo. Tunatazamia wakati ambapo majanga ya asili hayatakuwepo na badala yake kutakuwa na “wingi wa amani.”—Zaburi 37:11.