Hamia kwenye habari

INDIA

Maelezo Mafupi Kuhusu India

Maelezo Mafupi Kuhusu India

Mashahidi wa Yehova wamekuwapo nchini India tangu mwaka 1905. Walifungua ofisi yao mwaka 1926 katika jiji la Bombay (sasa Mumbai), na walisajiliwa rasmi kisheria mwaka 1978. Mashahidi wananufaika kutokana na sheria za katiba ya India inayompa watu haki ya kuabudu na kuwaambia wengine kuhusu imani yao. Ushindi wa kesi ya Bijoe Emmanuel dhidi ya Jimbo la Kerala uliotolewa na Mahakama Kuu ya India umechangia kwa kiasi kikubwa uhuru wa katiba unaowanufaisha wananchi wote. Kwa ujumla Mashahidi wa Yehova nchini India wana uhuru wa ibada. Hata hivyo, katika baadhi ya majimbo wameshambuliwa na vikundi vya watu wenye jeuri na kufanyiwa vitendo vingine vinavyotokana na ubaguzi wa kidini.

Katika mwaka wa 1977, Mahakama Kuu ilionyesha tofauti kati ya kutangaza dini na kubadili watu dini. Iliamua kwamba hakuna mtu mwenye haki ya kumbadili mtu mwingine dini na kwamba sheria zilizowekwa katika baadhi ya majimbo zinazopiga marufuku kuwabadili watu wengine dini ni halali. Wanapokamatwa na polisi, mara nyingi watu wanaowashambulia Mashahidi hurejelea uamuzi wa mahakama na kudai kwa uwongo kwamba waliwakuta Mashahidi wakibadili watu dini. Katika majimbo ambayo sheria inayokataza kubadili mtu dini haijawekwa, wapinzani hudai kwamba Mashahidi wanakufuru, wakitumia vibaya sheria iliyowekwa na wakoloni dhidi ya kazi ya kuhubiri inayofanywa na Mashahidi wa Yehova. Kwa sababu ya mashtaka hayo, Mashahidi wa Yehova wameshambuliwa zaidi ya mara 150 na makundi ya wafanya vurugu tangu mwaka 2002. Mara nyingi wenye mamlaka hufanya hali iwe mbaya zaidi kwa kuwa hawatoi ulinzi wa kutosha kwa wale wanaoshambuliwa na kuamua kutochukua hatua dhidi ya wanaofanya vurugu.

Mashahidi wa Yehova nchini India wanaendelea kuzungumza na maofisa wa serikali pamoja na kutuma maombi yao katika mahakama ili kulinda haki yao ya kuabudu kwa uhuru. Mashahidi wanatumaini kwamba wenye mamlaka na watu mmoja-mmoja watatii uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Bijoe: “Utamaduni wetu unatufundisha kuheshimu haki za wengine; falsafa yetu inahubiri kuheshimu haki za wengine; katiba yetu inaheshimu haki za wengine; nasi tufanye vivyo hivyo.” Mashahidi wanatumaini kwamba jitihada zao zitaondoa mashambulizi wanayofanyiwa na kwamba watu wengine wataheshimu haki yao ya kuabudu.