Hamia kwenye habari

AGOSTI 17, 2018
INDIA

Mmomonyoko Mbaya wa Udongo Kusini-mashariki mwa India

Mmomonyoko Mbaya wa Udongo Kusini-mashariki mwa India

Mvua kubwa zilinyesha katika jimbo la Kerala, nchini India, na kusababisha mmomonyoko wa udongo katika maeneo 25, na kuua watu 75 hivi. Kulingana na Idara ya Hali ya Hewa, msimu huu umekuwa na mvua nyingi zaidi kuwahi kurekodiwa katika eneo hilo.

Tumesikitika kusikia kutoka ofisi ya tawi ya India kwamba wenzi wa ndoa Mashahidi wenye umri wa miaka 60 hivi pamoja na mwanafunzi mmoja wa Biblia wamekufa kutokana na mmomonyoko wa udongo na wanafunzi wawili wa Biblia wamepata majeraha mabaya na wanaendelea kupata matibabu hospitalini. Pia, ndugu mwenye umri wa miaka 17 alikufa maji alipokuwa akijaribu kumwokoa jirani yake.

Halmashauri ya Kutoa Misaada (DRC) imeanzishwa ili kukagua madhara na kutoa msaada. Majumba fulani ya Ufalme yameteuliwa kuwa vituo vya kutoa msaada. Ripoti za awali zinaonyesha kwamba nyumba 46 hivi zimeharibiwa kwa kiasi fulani au kabisa. Familia 85 (wahubiri 475) wamehamia kwa muda kwenye nyumba za akina ndugu au watu wa ukoo. Imeripotiwa kwamba majumba fulani ya Ufalme yameingiwa na maji ya mafuriko. DRC inaendelea kuwa macho kwa sababu bado kunatarajiwa mvua kubwa katika siku zijazo.

Wawakilishi wa ofisi ya tawi, pamoja na mwangalizi wa mzunguko na wazee wa kutaniko waliwatembelea ndugu na dada zetu ili kuwafariji na kuwatia moyo kupitia Maandiko.

Tunawafikiria na kusali kwa ajili ya wote walioathiriwa na mvua hizo zilizosababisha madhara makubwa. Tunatazamia kwa hamu wakati ambapo misiba kama hiyo ya asili na maumivu yanayosababishwa na misiba hiyo, hayatakuwepo tena.—Ufunuo 21:3, 4.