OKTOBA 30, 2019
INDONESIA
Mahakama ya Indonesia Yalinda Uhuru wa Kidini wa Watoto wa Shule
Agosti 8, 2019, Mahakama ya Usimamizi ya Samarinda ilitoa uamuzi uliounga mkono msimamo wa watoto watatu waliofukuzwa shuleni kwa sababu ya kukataa kuisalimu bendera au kuimba wimbo wa taifa. Mahakama hiyo ilitoa agizo kwamba uamuzi wa kufukuzwa uondolewe na kwamba watoto hao watatu warudi shuleni. Uamuzi huo unathibitisha kwamba watoto hawapaswi kuadhibiwa kwa sababu ya kufuata usadikisho wa kidini wa wazazi wao ambao ni Mashahidi na kuonyesha kwamba sheria ya Indonesia inawaruhusu wazazi kuwapa watoto wao mwongozo wa kidini.
Yonatan, Yosua, na Maria Tunbonat, walio na umri wa miaka 7, 10, na 12 walifukuzwa shuleni Desemba 2018. Hata hivyo, Mahakama ya Usimamizi ilitambua kwamba watoto hao walipokataa kushiriki katika sherehe za kitaifa hawakutenda kinyume na Katiba au sheria; wala si kukosa heshima kwa tamaduni za kiraia au ishara za kitaifa.
Tunafurahi kwamba mahakama ilitoa uamuzi unaoheshimu msimamo wa watoto hao unaotegemea Biblia na kuwaruhusu waendelee na masomo yao. Tunatumaini kwamba uamuzi huo utawanufaisha pia watoto wengine Mashahidi nchini Indonesia wanaokabili changamoto hizo shuleni.