Hamia kwenye habari

JANUARI 14, 2020
INDONESIA

Mvua Yasababisha Mafuriko Makubwa Huko Jakarta

Mvua Yasababisha Mafuriko Makubwa Huko Jakarta

Inakadiriwa kwamba nyumba 100 za ndugu zetu zilifurika maji baada ya mvua kubwa kunyesha huko Jakarta, Indonesia, Desemba 31, 2019. Maji katika baadhi ya nyumba hizo yalifika kimo cha mita 1.5.

Ijapokuwa hakuna ndugu yetu hata mmoja aliyekufa au kujeruhiwa, wahubiri wengi walihitaji kuhama nyumba zao kwa muda fulani, na wengine ambao hawakuweza kuondoka walilazimika kutafuta sehemu salama ya kujikinga na maji hayo. Pia baadhi ya majengo yaliyotumiwa kwa ajili ya mikutano yalipata uharibifu mdogo. Wazee katika eneo hilo walifanya mipango ya kutoa msaada wa vitu muhimu kama vile chakula na maji. Vilevile, waangalizi wa mzunguko waliwatembelea wale walioathiriwa na msiba huo ili kuwapa faraja kutoka kwenye Maandiko. Halmashauri mbili za Kutoa Msaada zimeundwa ili kuchanganua msaada zaidi utakaohitajika.

Mafuriko hayo hayajawazuia ndugu zetu kuendelea na ratiba yao ya mambo ya kiroho, ingawa baadhi ya familia zilizoathiriwa zilihitaji kusafiri katika maeneo yaliyofurika ili kuhudhuria mikutano ya katikati ya juma. Ndugu Daniel Puromo, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Indonesia, alisema hivi: “Ingawa haya ndiyo mafuriko makubwa zaidi kutokea Indonesia katika miaka ya hivi karibuni, hilo halijawavunja moyo ndugu zetu, badala yake, limewachochea kusaidiana na kuonyeshana upendo wa Kikristo.”

Tunatarajia kwa hamu wakati ambapo nguvu zote za asili za dunia hazitasababisha madhara.—Marko 4:39.