JUNI 29, 2015
ISRAEL
Mahakama Kuu Nchini Israel Yatetea Haki ya Mashahidi ya Kukusanyika kwa Amani
IPolisi na Mahakama Kuu nchini Israel, yatetea uhuru wa ibada kwa kulinda haki ya Mashahidi wa Yehova ya kukusanyika ili kuabudu. Katika uamuzi wa hivi karibu, Mahakama Kuu iliamuru manispaa ya jiji la Ra’anana iheshimu mkataba wake na Mashahidi wa Yehova wa kukodisha ukumbi wa michezo wa Metro West Sports Center ili kufanyia makusanyiko mawili ya kidini. Baada ya kushinikizwa na vikundi fulani vya dini, manispaa ilivunja mkataba huo saa 36 kabla ya kuanza kwa kusanyiko la kwanza.
Mahakama Yapinga Uamuzi wa Manispaa Kuvunja Mkataba kwa Ubaguzi
Mashahidi wa Yehova waliingia mkataba na manispaa ya jiji la Ra’anana wa kufanya makusanyiko Aprili 18 na Mei 2, 2015. Mnamo Aprili 15, Mashahidi wa Yehova waligundua kwa mara ya kwanza kwamba huenda mkataba wa kufanya makusanyiko ukavunjwa baada ya meneja mkuu wa jiji kuzungumzia wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama wakati wa kusanyiko la Aprili 18. Ijapokuwa walihakikishiwa na mkuu wa polisi wa eneo hilo kwamba polisi watalinda usalama, manispaa ya jiji la Ra’anana ilivunja mkataba siku iliyofuata bila kuwahusisha Mashahidi. Vyombo vya habari vilisema kwamba manispaa ilifanya hivyo baada ya wajumbe wa manispaa wenye imani za dini kutishia kuacha kuiunga mkono kisiasa manispaa hiyo ikiwa ingewaruhusu Mashahidi wafanye makusanyiko yao.
Ingawa Mashahidi walifungua kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Lod ili kuilazimisha manispaa ya mji kuheshimu mkataba wao, hakukuwa na muda wa kutosha kuzuia kufutwa kwa kusanyiko la Aprili 18. Mashahidi walifanikiwa kukodi ukumbi mwingine ili kufanya kusanyiko lao na walilazimika kulipa mara sita zaidi ya bei waliyokubaliana kwenye mkataba wao na manispaa ya jiji kwa ajili ya ukumbi wa michezo.
Aprili 29, Mahakama ya Wilaya ya Lod ilitoa uamuzi na kuiamuru manispaa iheshimu mkataba wake ikisema kwamba “Manispaa ya [Ra’anana] ilivunja haki ya kikatiba ya [Mashahidi wa Yehova] ya uhuru wa ibada na desturi, uhuru wa kukusanyika, haki ya kuheshimiwa na kupewa uhuru na pia haki ya kutendewa kwa usawa.” Manispaa ya jiji ilikata rufaa ili kubatilisha uamuzi huo, lakini ombi hilo lilikataliwa na Mahakama Kuu mnamo Mei 1. Jitihada zaidi za kukata rufaa hazikufanikiwa na hivyo uamuzi wa mahakama ya wilaya unaendelea kutumika.
Polisi Wawalinda Mashahidi
Uamuzi huo uliotolewa wakati barabara na Mahakama Kuu uliwawezesha Mashahidi wa Yehova kufanya kusanyiko lao Mei 2. Viongozi wa dini, kutia ndani rabi mkuu wa jiji hilo na washiriki wenye msimamo mkali wa chama cha Othodoksi wanaojulikana kwa kufanya vurugu, walipanga kipindi cha “sala ya pamoja” kilichohudhuriwa na watu 1500 hivi baada ya uamuzi wa mahakama kutolewa. Watu hao walikusanyika mbele ya ukumbi wa michezo wakati uleule ambapo Mashahidi 600 walifika ili kuhudhuria kusanyiko. Baada ya muda mfupi, “sala ya pamoja” ikageuka na kuwa maandamano makubwa. Baadhi ya waandamanaji waliwashambulia Mashahidi—waliotia ndani wanawake na watoto. Waandamanaji hao waliwatukana, waliwatemea mate, waliwazomea, na kuharibu magari ya Mashahidi. Polisi waliingilia kati mara moja na kuwadhibiti waandamanaji. Kitendo hicho cha polisi, kiliwawezesha Mashahidi kufurahia kusanyiko lao na kurudi nyumbani wakiwa salama baada ya kusanyiko kuisha.
Mashahidi wa Yehova nchini Israel wanawashukuru wenye mamlaka waliopinga chuki na ubaguzi wa kidini kwa kutetea haki yao ya kukusanyika ili kuabudu kwa amani.