Hamia kwenye habari

Jengo la Palace of Justice huko Rome, lililo na Mahakama Kuu ya Italia

OKTOBA 1, 2019
ITALIA

Mahakama Kuu ya Italia Yaunga Mkono Haki Sawa za Kuwafundisha Watoto Kuhusu Dini Katika Kesi za Kutunza Watoto

Mahakama Kuu ya Italia Yaunga Mkono Haki Sawa za Kuwafundisha Watoto Kuhusu Dini Katika Kesi za Kutunza Watoto

Mnamo Agosti 30, 2019, Mahakama Kuu huko Rome, ilitoa uamuzi muhimu wa kisheria unaohusiana na kutunza watoto. Mahakama hiyo ya juu zaidi nchini Italia ilitoa uamuzi uliounga mkono haki ya mama mmoja, ambaye ni Shahidi wa Yehova, kumfundisha mtoto wake mafundisho yake ya kidini.

Baba ya mtoto huyo ambaye si shahidi, alitengana na mke wake, na kusisitiza kwamba mtoto afundishwe tu kuhusu itikadi za kidini za baba yake. Mahakama mbili za mwanzoni zilitoa uamuzi uliomuunga mkono baba huyo, na kusema kwamba kumfundisha mtoto huyo dini nyingine kungefanya “achanganyikiwe.” Maamuzi hayo yaliingilia haki ya mama yake ya kumfundisha mwanaye kuhusu imani yake ya kidini. Mahakama Kuu ilitoa uamuzi ulio kinyume na mahakama za mwanzoni na kusisitiza haki ya mtoto huyo ya “kushirikiana kwa usawa na wazazi wote wawili.” Vilevile mahakama hiyo ilikazia kwamba dini zote “zinapaswa kutendewa kwa usawa kisheria” na kukashifu kile ilichosema ni “ubaguzi” kuwaelekea Mashahidi wa Yehova uliofanywa na mahakama za chini. Uamuzi huo unathibitisha kwamba iwapo maoni ya wazazi yanatofautiana kuhusu elimu ya kidini ambayo watawapa watoto wao, hakimu hana haki ya kuwaamulia dini iliyo bora.

Tunatumaini kwamba uamuzi wa Mahakama hiyo utaweka msingi kwa ajili ya kesi za wakati ujao zinazohusu kuwatunza watoto nchini Italia. Bila shaka hilo litawasaidia wazazi wanaojitahidi kuwalewa watoto wao katika “nidhamu na maagizo ya Yehova.”—Waefeso 6:4.