NOVEMBA 12, 2020
ITALIA
Mahakama Nchini Italia Yaunga Mkono Haki ya Wazazi Mashahidi ya Kuamua Matibabu ya Watoto Wao
Hivi karibuni, Mahakama ya Rufaa katika jiji la Milan, Italia, ilitoa uamuzi unaotetea wenzi wa ndoa Mashahidi wa Yehova katika kesi iliyohusu matibabu ya mtoto wao. Uamuzi huo unasaidia kuweka msingi kwamba mahakama hazipaswi kutilia shaka uwezo wa wazazi ikiwa wataomba watoto wao wasipewe matibabu yanayohusisha kutiwa damu mishipani kwa sababu ya imani yao ya kidini.
Septemba 2019, wenzi wa ndoa Mashahidi walimpeleka hospitalini binti yao aliyekuwa na umri wa miezi kumi aliyeumia kutokana na jeraha alilopata baada ya kuanguka. Madaktari waligundua kwamba binti huyo alihitaji kufanyiwa upasuaji ili kutibu jeraha hilo. Madaktari walifanikiwa kumfanyia upasuaji bila ya kumtia damu mishipani.
Baadaye, ingawa binti huyo alikuwa akipata nafuu na hakuwa katika hatari yoyote, daktari mmoja aliwaomba wazazi wa binti huyo ruhusa ya kumtia damu mtoto huyo kama “tiba ya kumsaidia.” Wazazi hao waliomba kwamba mtoto wao atibiwe kwa kutumia mbinu nyingine ambazo kwa ukawaida hutumiwa na hazihusishi damu.
Badala ya kukubali ombi la wazazi hao, daktari huyo alizungumza na polisi na ofisi ya mwendesha-mashtaka. Ofisi ya mwendesha-mashtaka ilifanikiwa kupata amri ya mahakama kutoka katika mahakama ya familia. Kulingana na sheria, amri hiyo ya mahakama inazuia mamlaka ya wazazi na kumpa mkurugenzi wa hospitali mamlaka ya kuamua matibabu ya mtoto. Hata hivyo, mtoto huyo hakutiwa damu kwa sababu madaktari waliamua kwamba haikuwa lazima kufanya hivyo.
Tukio hilo lilizungumziwa sana katika vyombo vya habari nchini humo. Vyombo vingi vya habari nchini Italia vilitoa taarifa zisizo za kweli kuwa uhai wa msichana huyo uliokolewa baada ya mahakama kutoa amri ya kwamba atiwe damu mishipani.
Septemba 10, 2020, Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali uamuzi wa mahakama ya familia wa kuzuia mamlaka ya wazazi. Mahakama ya Rufani ilisema kwamba mahakama ya familia haikupaswa kutoa amri na haikuwa na mamlaka ya kuamua kesi hiyo.
Katika uamuzi huo, Mahakama ya Rufaa ya Milan ilisema hivi: “Hatua ya wazazi ya kukataa mtoto wao kutiwa damu kulingana na imani yao ya kidini, haikupaswa kuwa msingi wa kuamua kwamba hawana uwezo wa kutimiza jukumu lao wakiwa wazazi.” Mwaka jana pekee, Mahakama tatu za Rufaa nchini Italia ziliunga mkono haki ya wazazi Mashahidi ya kuchagua matibabu yasiyohusisha damu kwa niaba ya watoto wao.
Ni muhimu kwa mamlaka za mahakama na madaktari kujua kwamba Mashahidi wa Yehova hawaamini kwamba wataponywa kimuujiza na kwamba hawatumii dawa. Kwa kweli, Mashahidi wa Yehova wanapenda kupata huduma bora za matibabu katika hospitali za kisasa zilizo na madaktari wazoefu wanaotoa tiba kulingana na imani yao ya kidini. Mashahidi wanawaomba madaktari kutowatia damu mishipani wanapowatibu. Madaktari wengi maarufu walio katika hospitali kubwa ulimwenguni pote wamekubali ombi hilo na wanaendelea kuwapatia tiba bora bila ya kutumia damu.
Tunathamini sana kwamba maamuzi hayo ya mahakama huwategemeza ndugu na dada zetu wanapoendelea kudumisha azimio lao la kukubali matibabu yanayofaa kwa ajili ya watoto wao.—Matendo 15:29.