Hamia kwenye habari

Mahakama ya Rufaa ya Rome

FEBRUARI 7, 2020
ITALIA

Mahakama ya Rufaa ya Rome Yaunga Mkono Haki ya Wazazi ya Kuamua Watoto Wao Wapewe Matibabu Yasiyohusisha Damu

Mahakama ya Rufaa ya Rome Yaunga Mkono Haki ya Wazazi ya Kuamua Watoto Wao Wapewe Matibabu Yasiyohusisha Damu

Desemba 17, 2019, Mahakama ya Rufaa ya Rome ilibatilisha hukumu iliyotolewa na mahakama ya kesi za watoto nchini Rome ambayo ilimnyang’anya dada yetu haki ya kulea mtoto wake kwa kuwa hakuruhusu mwana wake atiwe damu. Mahakama ya Rufaa ilimrudisha mtoto kwa mama yake na hata kufuta mashtaka hayo. Uamuzi huo unaweka msingi mzuri wa kisheria kwa ajili ya kesi nyingine kama hizo, na pia inawahakikishia wazazi ambao ni Mashahidi kwamba hawatapoteza haki yao ya kulea watoto wao kwa sababu ya kuchagua matibabu yasiyohusisha damu.

Kesi hiyo ilianza dada yetu alipopata aksidenti pamoja na mwana wake mwenye umri wa miaka kumi. Mtoto huyo aliumia hivyo akapelekwa hospitalini. Baada ya siku tatu, madaktari walifanya mipango ya kumfanyia upasuaji. Dada yetu alikubaliana na upasuaji huo pamoja na njia zao zote za matibabu, lakini pia, aliwaambia kwamba hatakubali wamtie damu mishipani. Ingawa mwana wake hakuhitaji matibabu yanayohusisha damu, hospitali hiyo iliamua kumshtaki dada huyo kwa kosa la kutojali afya ya mwana wake kwa sababu za kidini. Pia waliomba wamtie damu mishipani ikiwa hali ingebadilika. Mwendesha mashtaka alisema kwamba dada yetu hakufikiria hali njema ya mwanaye kisha akaomba mahakama ya kesi za watoto imnyang’anye haki yake ya kumlea. Mahakama ya kesi za watoto ilikubali ombi lake licha ya kwamba haina mamlaka ya kisheria ya kuamua juu ya suala hilo. Hivyo basi, dada yetu alikata rufaa juu ya uamuzi huo kwenye Mahakama ya Rufaa.

Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba dada yetu ni mama mzuri anayemjali mwana wake. Uamuzi huo ulisema kwamba “kwa kuwa alikataa tu kumtia mwanaye damu, kwa sababu za kidini, si jambo linalodhihirisha kwamba yeye si mzazi asiyeweza kumlea mwana wake.” Mahakama hiyo ilimrudishia dada huyo haki yake ya kulea watoto na kutangaza kwamba uamuzi wa mahakama hiyo ulikuwa na makosa.

Nicola Colainni, aliyewahi kuwa mshauri wa Mahakama Kuu na profesa wa sheria za kanisa katika Chuo Kikuu cha Bari, alisema hivi: “Ninakubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa. Ninashangazwa na hukumu zilizotolewa kama hukumu ya mahakama ya kesi za watoto. Ni wazi kwamba ni vigumu sana kwa watu kufurahia uhuru wao wa kidini, na ni vigumu hata zaidi kwa Mashahidi wa Yehova.”

Ndugu Christian Di Blasio, anayeratibu kazi za Dawati la Habari za Umma nchini Italia alisema hivi: “Tunaishukuru Mahakama ya Rufaa ya Rome kwa kubatilisha uamuzi uliochochewa na ubaguzi wa kidini. Mashahidi wa Yehova hujali watoto wao sana na wanathamini kazi ya madaktari wengi wanaowapa huduma bora kabisa huku wakizingatia dhamiri yao ya Kikristo.”

Uamuzi huu wa mahakama unawahakikishia akina ndugu na dada kwamba wana haki ya kufanya maamuzi yanayohusiana na afya za watoto wao. Tunamshukuru Mungu wetu, Yehova, kwa ushindi tuliopata mahakamani, ambao utasaidia waabudu wenzetu wanapofanya maamuzi yanayohusiana na afya kulingana na dhamiri zao za Kikristo.—Zaburi 37:28.