NOVEMBA 16, 2020
ITALIA
Mradi wa Kuhamisha Ofisi ya Tawi ya Italia Waendelea Licha ya Changamoto
Licha ya changamoto za kiuchumi na kiafya, mradi wa kuhamisha ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Italia kwenda katika jiji la Bologna, unaendelea. Septemba 5, 2020, mradi huo ulipiga hatua kubwa jengo la kwanza la makazi lilipomalizika. Ujenzi wa ofisi mpya ya tawi umepangwa kumalizika mwishoni mwa 2023.
Halmashauri ya Mradi wa Ujenzi (CPC) iliyo na ndugu watano inasimamia ujenzi wa ofisi hiyo mpya. Kandarasi alipewa mradi huo ili kubuni na kujenga jengo hilo la makazi, kazi iliyoanza Septemba 2018.
Katika mwaka wa 2019, hali mbaya ya kiuchumi ilikumba kampuni nyingi katika eneo hilo. Hali hiyo ililazimisha kandarasi asimamishe kazi na kujipanga upya. Inapendeza kwamba ujenzi wa jengo la makazi tayari ulikuwa umemalizika na hivyo kuwezesha kazi iendelee baada ya kusimama kwa muda mfupi.
Mwanzoni mwa mwaka wa 2020, ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ulikumba eneo la kaskazini mwa Italia, kutia ndani jiji la Bologna. Wenye mamlaka walitoa amri ya kusitishwa kwa shughuli nyingi katika jiji kutia ndani miradi ya ujenzi. Hata hivyo, baada ya mwezi mmoja, wenye mamlaka waliondoa baadhi ya vizuizi na kazi iliweza kuendelea kwa kuzingatia miongozo ya afya na tengenezo letu ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona.
Ndugu Paolo Comparato, mshiriki wa CPC, alisema hivi: “Tunamshukuru Yehova kwa kutusaidia kumaliza jengo hili. Bila ya roho yake, tusingeweza kukabiliana na changamoto zote tulizopata.”
Bi. Cristina Dallacasa, mwenyekiti wa kandarasi inayosimamia ujenzi, alisema hivi: “Tunafurahi kwamba Mashahidi wa Yehova waliamua kujenga majengo yao muhimu sana hapa Italia. Tunafanya kazi pamoja kama timu, na jambo hilo limetuwezesha kukabiliana na changamoto zote zilizojitokeza wakati wa ujenzi. Mashahidi wa Yehova wamethibitisha kwamba wanajali sana miradi yao, na hasa usalama wa wale wanaohusika katika ujenzi.” Anamalizia kwa kusema: “Zaidi ya yote, ninashukuru sana kupata nafasi ya kufanya kazi na kikundi cha watu wanyoofu na wanaotegemeka. Katika wakati huu wenye misukosuko ya kijamii na kiuchumi, sifa hizo ni za muhimu sana.”
Tuna uhakika kwamba Yehova ataendelea kutegemeza mradi huu ili ulete heshima kwa jina lake.—Zaburi 127:1.