Hamia kwenye habari

Jengo la ofisi lenye orofa tisa likifanyiwa marekebisho huko Bologna, Italia

OKTOBA 23, 2019
ITALIA

Ujenzi wa Ofisi Mpya ya Tawi Nchini Italia

Ujenzi wa Ofisi Mpya ya Tawi Nchini Italia

Jengo lililo Imola, ambalo linatumiwa na Idara ya Utafsiri

Ofisi ya tawi ya Italia inahamisha majengo yake kutoka Rome kwenda kwenye majiji ya Bologna na Imola. Jiji la Bologna liko kilomita 370 hivi kaskazini mwa Rome, nalo jiji la Imola liko kilomita 48 hivi kutoka Bologna. Tayari marekebisho yameanza kufanywa katika jengo la orofa tisa lililo huko Bologna ambalo litatumika kama ofisi. Kufikia mwaka wa 2018, zaidi ya wajitoleaji 60 walio Betheli wanaofanya kazi ya utafsiri na kazi nyingine katika idara hiyo wamekuwa wakifanya kazi katika jengo jipya lililorekebishwa huko Imola.

Ili kuandaa makazi kwa ajili ya Wanabetheli watakaohamia Bologna, jengo la makazi lenye orofa saba na orofa tatu za maegesho zilizo chini ya ardhi linajengwa karibu kilomita moja na nusu kutoka kwenye jengo la ofisi. Baadaye kutakuwa na majengo ya ziada ya makazi katika eneo hilo.

Mchoro unaoonyesha jengo la makazi lenye orofa saba ambalo linajengwa

Mwaka wa 1948, Mashahidi wa Yehova walinunua jengo la kwanza la ofisi ya tawi huko Rome na kuhamishia utendaji wao huko kutoka kwenye majengo yaliyokuwa Milan. Tangu wakati huo, nchi ya Italia imekuwa na ongezeko la ajabu. Katika miaka ya 1940, kulikuwa na wahubiri wasiozidi 200 nchini humo. Leo, kuna zaidi ya wahubiri 250,000, idadi kubwa zaidi ya wahubiri katika ofisi za tawi zilizo barani Ulaya. Kadiri idadi ya wahubiri katika eneo la ofisi hiyo ya tawi ilivyozidi kuongezeka, ndivyo idadi ya wajitoleaji wa Betheli na majengo ya ofisi ya tawi ilivyozidi kuongezeka. Mwaka wa 2006, ofisi ya tawi ya Italia ilikuwa na kilele cha jumla ya majengo 99. Baada ya utendaji wake wote kuunganishwa, ofisi hiyo ya tawi itakuwa na idadi ndogo ya Wanabetheli na jumla ya majengo matano tu.

Tunasali kwamba Yehova aendelee kubariki mradi huu na kwamba majengo hayo mapya yaendelee kutegemeza kazi inayofanywa nchini Italia, shamba ambalo ni ‘jeupe kwa ajili ya kuvunwa.’—Yohana 4:35.