Hamia kwenye habari

Ofisi ya Mwendesha-mashtaka wa Serikali na mahakama ya Termini Imerese jijini Sicily, Italia.

AGOSTI 22, 2018
ITALIA

Mahakama Jijini Sicily Yathibitisha Haki ya Kujiamulia ya Wagonjwa Mashahidi wa Yehova

Mahakama Jijini Sicily Yathibitisha Haki ya Kujiamulia ya Wagonjwa Mashahidi wa Yehova

Aprili 6, 2018, Mahakama ya Termini Imerese jijini Sicily, Italia, ilitoa uamuzi kwamba daktari wa upasuaji aliyemlazimisha mwanamke ambaye ni Shahidi wa Yehova atiwe damu mishipani, anapaswa kujibu mashtaka ya uhalifu. Daktari huyo aliagizwa alipe fidia ya dola 11,605 za Marekani kwa mwanamke huyo, na dola 5,803 za Marekani kwa mume wa mwanamke huyo ambaye pia ni Shahidi wa Yehova. Huo ni uamuzi wa kwanza katika mahakama ya Italia ambao umemhukumu daktari kwa uhalifu kwa sababu ya kuvunja haki ya msingi ya mgonjwa ya kuamua jinsi mwili wake utakavyotibiwa kupatana na imani yake.

Kesi hiyo ilimhusu dada ambaye alianza kupata matatizo baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifuko cha nyongo uliofanywa Desemba 2010. Ingawa alikataa kutiwa damu mara kadhaa, alifungwa na kutiwa chembe nyekundu kwa nguvu. Daktari huyo wa upasuaji alidai kwa uwongo kwamba alipata mamlaka kutoka kwa jaji.

Kwa hiyo, yeye na mume wake walituma malalamiko kwenye Ofisi ya Mwendesha-mashtaka wa Serikali. Mahakama iliamua kwamba “ikiwa Shahidi wa Yehova ana umri wa kutosha kisheria na ana uwezo wa kujifanyia uamuzi mwenyewe, . . . daktari hapaswi kumpa matibabu hayo” yanayopingana na mapendezi ya mgonjwa.

Mahakama pia ilitangaza kwamba Katiba ya Italia inawakataza madaktari kutoa matibabu bila kibali cha mgonjwa hata ikiwa daktari anaona matibabu hayo kuwa ya lazima. Kulingana na uamuzi wa mahakama, “uamuzi wa kwamba matibabu ni ya lazima . . . hautumiki ikiwa mgonjwa ameeleza wazi na kwa uhuru kwamba hataki matibabu hayo.”

Daniele Rodriguez, profesa wa Kitengo cha Sheria cha Masuala ya Kitiba na Maadili katika Chuo Kikuu cha Padua na shahidi wa utaalamu, alisema katika ripoti ya kitiba aliyoandika kwa ajili ya kesi hiyo, kwamba “haki ya kukataa matibabu fulani inalindwa na sheria za katiba na ikawekwa wazi na [kifungu cha] 32 cha Katiba ya [Italia] inayosema kuwa ‘hakuna anayelazimishwa kufuata tiba yoyote isipokuwa sheria iwe inasema kwamba ni lazima.’” Luca Benci, jaji wa Italia na mtaalamu wa sheria za afya, aliandika hivi kuhusu uamuzi wa mahakama katika jarida Quotidiano Sanità (Health Daily): “Hakuna sheria inayolazimisha wagonjwa watiwe damu bila hiari yao. Haki ya kukataa matibabu ni muhimu kuliko mambo mengine yanayopaswa kuzingatiwa.”

Marcello Rifici, wakili mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alisema hivi: “Tunafurahi kwamba uamuzi huu unakubaliana na viwango vilivyowekwa vya Ulaya, kama vile vilivyotolewa katika uamuzi wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu, ambavyo vinadumisha haki ya wagonjwa wote ya kujiamulia matibabu. Inapendeza kwamba katika mwaka wa 2017 Bunge la Italia lilitunga sheria ya 219/2017, inayojulikana kama ‘Haki ya Kisheria ya Anayeishi,’ ambayo inataja kanuni zilezile kama uamuzi uliotolewa.”

Lucio Marsella, ambaye pia alikuwa wakili wa Mashahidi, alisema: “Uamuzi huo utakuwa msingi wa kuwatetea madaktari wote wanaofanya kazi kwa kudhamiria na kwa ujasiri ili kuwatibu wagonjwa kwa njia bora zaidi huku wakiheshimu uhuru wao wa kuchagua.”