JUNI 27, 2019
ITALIA
Madaktari Katika Makongamano Mawili Makubwa ya Kitiba Nchini Italia Wapendezwa na Matibabu Yasiyohusisha Damu
Madaktari wengi wameonyesha kwamba wanathamini mfumo wa ulimwenguni pote unaotumiwa na tengenezo letu ili kuandaa habari kuhusu mbinu za matibabu na za upasuaji zisizohusisha kutiwa damu mishipani. Idara ya Huduma za Habari za Hospitali (Italia), katika ofisi ya tawi iliyoko Rome, ni sehemu ya mfumo huo wa ulimwenguni pote. Mwishoni mwa mwaka uliopita, wawakilishi wa Idara ya Huduma za Habari za Hospitali (Italia) na washiriki wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali walisimamisha kibanda cha maonyesho katika Kongamano la Kitaifa la Shirika la Italia la Nusu-kaputi, Kupunguza Maumivu, Kusaidia Kupumua, na Kushughulikia Wagonjwa Mahututi (SIAARTI), lililofanywa kuanzia Oktoba 10 hadi 13, 2018, huko Palermo, Sicily. Baada tu ya kongamano hilo, ndugu pia walishiriki maonyesho katika Kongamano la Mashirika ya Kisayansi ya Upasuaji lililofanyiwa huko Rome katika Kituo cha Kusanyiko cha “La Nuvola.”
Makongamano kama hayo yanaandaa fursa za kutoa habari za karibuni zaidi za matibabu yasiyohusisha damu kwa wataalamu wengi wa kitiba wanaopendezwa kwa wakati uleule. Kongamano la Palermo lilihudhuriwa na madaktari 2,800 wa nusu-kaputi. Kongamano la Rome, ambalo linaonwa kuwa kongamano kubwa zaidi kuhusu upasuaji kuwahi kufanywa nchini Italia, lilihudhuriwa na madaktari wa upasuaji 3,500. Wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali zinazoheshimiwa pia walihudhuria. Walitia ndani washiriki kutoka mashirika yote ya madaktari wa upasuaji na kutoka Chuo cha Marekani cha Madaktari wa Upasuaji Kitengo cha Italia. Taasisi za kitaifa kama Wizara ya Afya, zilifadhili tukio hilo.
Daktari wa nusu-kaputi, Vincenzo Scuderi, kutoka Hospitali ya Policlinico iliyoko Catania, Sicily, alitembelea kibanda chetu cha maonyesho katika kongamano la Palermo. Januari 18, 2019, alimfanyia upasuaji wa dharura mgonjwa Shahidi ambaye mshipa wake mkubwa wa damu moyoni ulipasuka. Alifaulu kumaliza upasuaji huo tata bila kutumia damu. Dakt. Scuderi anaeleza hivi: “[Kibanda chenu cha maonyesho] katika Kongamano la SIAARTI la 2018 kilinisaidia sana kufanikiwa katika upasuaji huo. Habari nilizopewa hapo zilinisaidia sana.”
Kwa sasa, madaktari zaidi ya 5,000 nchini Italia wamekubali kuwatibu wagonjwa ambao ni Mashahidi wa Yehova kwa kutumia mbinu salama na zinazofaa za kitiba na za upasuaji ambazo hazihusishi kutia damu mishipani. Kila mwaka nchini Italia, Mashahidi 16,000 hivi wanatibiwa kwa njia hiyo.