JANUARI 2, 2020
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Mafuriko Yaenea Kwa Kasi Nchini Kongo
Vimbunga na mafuriko yamefanya hali iwe tete katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo huko Afrika ya Kati. Ofisi ya Tawi ya Mashahidi wa Yehova iliyo Kongo (Kinshasa) imeripoti kwamba Mashahidi wengi wameathiriwa na mafuriko hayo. Kwa kusikitisha, mmoja kati ya ndugu zetu anayeishi katika mji mkuu wa Kinshasa, alikufa maji.
Ofisi ya Tawi ya Kongo (Kinshasa) imewasilisha ripoti hii:
Katika mkoa wa kusini-magharibi wa Kasai, upepo mkali ulioambatana na mvua kubwa uliharibu nyumba za Mashahidi wenye familia zao.
Jumba la Ufalme lililo katika mkoa wa kaskazini-magharibi wa Sud-Ubangi lilikuwa limefurika maji ya mvua. Jengo hilo lilitumiwa na makutaniko matatu yenye jumla ya wahubiri 69. Mafuriko hayo yaliathiri familia 22 katika eneo hilo pia. Ofisi ya tawi ilichagua painia wa pekee na mzee mwingine ili kufanya mipango ya kuwaandalia mahitaji ya kimwili na kiroho ndugu na dada walio katika maeneo ya mbali yaliyoathiriwa na janga hilo.
Katika mkoa wa Tshopo, ndugu na dada walioishi pembezoni mwa Mto Congo wamelazimika kuhama eneo hilo. Kwa kuongezea, Majumba kadhaa ya Ufalme yaliyo katika eneo hilo yalifurika maji ya mvua.
Makutaniko yaliyo katika mji mkuu wa Kinshasa, yameripoti kwamba familia 80 hivi zimeathiriwa na mafuriko.
Kwa kuwa mafuriko hayo yamesababisha uchafuzi wa mazingira ambao umeongeza uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko, ofisi ya tawi inawafundisha wahubiri jinsi ya kulinda afya zao.
Licha ya changamoto wanazokabili, ndugu na dada wanasaidiana mahitaji ya msingi kama vile chakula na nguo. Pia Halmashauri za Kutoa Misaada, chini ya mwongozo wa ofisi ya tawi, zinatoa msaada kwa akina ndugu.
Tunajua kwamba sala zetu, pamoja na msaada wa kimwili na wa kiroho unaoandaliwa na tengenezo la Yehova, utaleta ‘faraja kwa wote wanaoomboleza’ katika nyakati hizi ngumu kushugulika nazo.—Isaya 61:1, 2.