Hamia kwenye habari

Ramani inayoonyesha mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Msichana akinawa mikono katika kusanyiko la mzunguko la Beni.

MEI 2, 2019
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Ugonjwa Hatari wa Ebola Waenea Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Ugonjwa Hatari wa Ebola Waenea Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Katika kipindi hiki cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, kumekuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulioanza Agosti 2018. Imeripotiwa kwamba watu zaidi ya 1,088 wamepata Ebola na watu 665 wamekufa katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Ituri. Inasikitisha kwamba ndugu zetu wameathiriwa na ugonjwa huo. Ofisi ya tawi ya Kongo (Kinshasa) imeripoti kwamba kati ya Mashahidi wa Yehova, watu wazima kumi na watoto watatu wamekufa kutokana na ugonjwa huo. Kuna ndugu mmoja aliyeambukizwa lakini ameshapona.

Ili kuwaelimisha akina ndugu kuhusu jinsi ya kuzuia ugonjwa huo, ofisi ya tawi ya Kongo (Kinshasa) ilipata kibali kutoka kwa Halmashauri ya Waratibu kutayarisha video ya pekee na hotuba. Video hiyo inatoa mapendekezo yanayofaa kuhusu kuweka sehemu za kunawa mikono, jambo ambalo makutaniko yote yametekeleza. Hatua hizo zimesaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo. Kwa sababu hiyo, maofisa wawili wa afya ya umma walichochewa kutuma barua kwenye ofisi ya tawi wakithamini mwenendo mzuri na ushirikiano unaoonyeshwa na Mashahidi wa Yehova wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.—Mathayo 5:16.

Katika majiji mengi, ndugu zetu wamezuiwa kuondoka nyumbani kwao kwa majuma kadhaa. Ili kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo katika kipindi hiki chenye msukosuko, ofisi ya tawi imeomba mizunguko 12 iahirishe makusanyiko yao ya eneo. Ili kuhakikisha kwamba akina ndugu bado wanapata chakula cha kiroho, ofisi ya tawi imefanya mipango ili makutaniko yaliyoathiriwa yatazame video iliyorekodiwa ya programu ya kusanyiko katika Majumba yao ya Ufalme.

Tunasali kwa ajili ya ndugu na dada zetu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tunajipa ujasiri kutokana na tumaini la Biblia kuhusu wakati ujao ambapo ugonjwa hautakuwepo tena.—Isaya 33:24.