JULAI 18, 2018
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Ndugu Kaskazini-Mashariki mwa Kongo Wakimbia Vita
Tangu Desemba 2017, vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jamii za Hema na Lendu katika mkoa wa Ituri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimesababisha vifo vingi na makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia. Ndugu wengi ni kati ya wale walioathiriwa na jeuri hiyo inayoongezeka.
Maelfu ya wakimbizi wa Kongo wamekimbilia nchini Uganda ili watoroke vita hivyo, kutia ndani wahubiri 192 ambao wanaishi katika kambi mbili za wakimbizi karibu na mpaka wa Kongo. Kufikia Juni 2018, Mashahidi wengine 1,098 walikuwa wamekimbia eneo la vita na kwenda Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri. Inasikitisha kwamba wenzi wa ndoa pamoja na watoto watatu ambao wazazi wao ni wahubiri waliobatizwa, walikufa kwa sababu ya matatizo ya kiafya. Hata hivyo, hakuna ndugu au dada aliyeuawa katika vita hivyo vya kikatili.
Nyumba nyingi za ndugu waliokimbia vita zimeporwa au kuteketezwa. Pia, mazao ambayo akina ndugu walipanda ili kujikimu yameharibiwa.
Kuanzia wakati ambapo vita vilianza, wahubiri katika maeneo salama waliwasaidia ndugu walioathiriwa. Baadhi yao waliwapa magari ya kuwasafirisha katika eneo salama (tazama picha kuu). Isitoshe, familia 205 katika eneo la Bunia walitoa pesa, chakula, na kuwapa makao ndugu waliokimbia, ingawa wao wenyewe walikuwa maskini. Ingawa kuna kambi mbili kubwa katika eneo la Bunia, wahubiri wote waliokimbia wamepewa makao na Mashahidi wenyeji.—Methali 17:17.
Halmashauri ya Tawi nchini Kongo imeanzisha Halmashauri ya Kutoa Msaada ambayo imewaandalia ndugu na dada mahitaji ya msingi. Mwakilishi wa ofisi ya tawi aliwatembelea ndugu walioathiriwa na kuwatia moyo kiroho.
Licha ya kwamba wamepoteza makao, ndugu na dada waliokimbilia Bunia na maeneo mengine wanakusanyika kwa ajili ya ibada na makutaniko ya eneo hilo na wanashiriki kwa bidii kutangaza habari njema pamoja na wengine. Kuanzia Februari hadi Aprili 2018, ndugu wameanzisha mafunzo 270 katika kambi za wakimbizi.
Tunasali kwamba Yehova ataendelea kuwapa amani ya akili ndugu na dada zetu nchini Kongo na kubariki kazi ya kutoa msaada. Kila mmoja wetu anatazamia kwa hamu siku ambayo Ufalme wa Mungu utakuja na kuandaa usalama wa kudumu na kuwapa watu wote wa Yehova “mahali pa kupumzika penye utulivu.”—Isaya 32:17, 18..