MACHI 12, 2015
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Yakataza Ubaguzi wa Kidini Shuleni
“Vita dhidi ya ubaguzi na ukosefu wa usawa ni jambo [muhimu] katika Elimu ya Taifa.”— Ofisi za Katibu wa Wizara ya Elimu, Juni 12, 2014.
Kwa miaka kadhaa, watoto wa Mashahidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekuwa wakifukuzwa kutoka katika shule zinazoendeshwa na mashirika ya dini nyingine kwa sababu ya kutoshiriki katika programu zao za kidini. Hilo lilikuwa suala zito kwa sababu shule hizo zimeweka sheria za juu kuliko zile za serikali na hivyo kukiuka haki za wanafunzi Mashahidi. Serikali ya DRC iliona ukosefu huo wa haki na kutetea haki ya wote ya kupata elimu bila ubaguzi.
Shule Zinazoendeshwa na Makanisa Zafuata Sheria Zao Badala ya za Serikali
Mashirika ya kidini yamefanya mikataba na serikali ya DRC ili kudhamini shule za umma katika maeneo yenye uhitaji. Mikataba hiyo inaeleza wazi kwamba “watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya matendo yanayochochea ubaguzi wa kidini.” Hata hivyo, shule hizo zinazoendeshwa na makanisa, zilikuwa na sheria za shule zilizowalazimisha wanafunzi kuhudhuria na kushiriki katika programu za kidini. Shule kadhaa zilisisitiza sheria zao zifuatwe, na hivyo kupuuza mkataba wao na serikali pamoja na haki ya wanafunzi ya uhuru wa kuabudu.
Tatizo hilo lilionekana wazi mwaka wa 2005, wanafunzi 52 ambao ni Mashahidi walipofukuzwa kutoka katika shule inayoendeshwa na kanisa katika kijiji cha Abumombazi, Jimbo la Equateur, kwa sababu waliomba kutoshirikishwa katika vipindi vya ibada vilivyopangwa na mamlaka za shule. Tatizo liliongezeka baada ya shule nyingine zinazoendeshwa na kanisa kufanya vivyo hivyo. Baada ya muda, Mashahidi 300 Wakongomani wa madarasa tofauti-tofauti kutia ndani waliokaribia kuhitimu, wakafukuzwa.
Kanyere Ndavaro, mwenye umri wa miaka 13, aliyefukuzwa isivyo haki katika mwaka wa 2009 aliandika hivi: “Ninasikitika sana kwamba nimeharibiwa maisha yangu. Sijui wakati wangu ujao utakuwaje.” Kambere Mafika Justin, aliyefukuzwa muda mfupi kabla ya kuhitimu mwaka wa 2010, alisema kuwa maisha yake “yameharibiwa kabisa.” Ingawa wanafunzi hao walisikitishwa na kitendo hicho cha kunyimwa elimu au diploma, walikataa kulegeza imani yao.
Maofisa Nchini DRC Watetea Uhuru wa Kidini
Wazazi wa watoto waliofukuzwa walizungumza na wasimamizi wa shule ili kutatua tatizo hilo lakini hawakufanikiwa. Hivyo, Mashahidi hao walifikisha suala hilo serikalini na kuzungumza na maofisa wasio na ubaguzi waliofanya jitihada za kukomesha ubaguzi huo wa kidini.
Mwaka wa 2011, Waziri wa Elimu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Bi. Bazizane Maheshe, alichapisha barua yenye kichwa “Ubaguzi wa Kidini Wapigwa Marufuku,” ambayo ilisema matendo hayo ni “mabaya sana.” Barua hiyo ilizungumzia suala hilo waziwazi kwa kusema hivi: “Wanafunzi wa baadhi ya dini nyingine wanabaguliwa kwa misingi ya sheria za shule zinazokiuka sheria zinazotumika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.”
Suala hilo lilifikia hatua ya kitaifa Septemba 4, 2013, Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mwangu Famba, alipotoa amri iliyopaswa kufuatwa na shule katika wilaya zote nchini. “Barua juu ya Ubaguzi wa Kidini Wapigwa Marufuku” ilisema hivi waziwazi: “Watoto wote wana haki ya kujiandikisha katika shule yoyote bila kubaguliwa kwa msingi wa dini.” Amri hiyo ilieleza pia kwamba kuwafukuza wanafunzi kwa misingi ya dini ni “kinyume kabisa na viwango na sheria zinazotumika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.”
Shule nyingi zimetii miongozo hiyo rasmi na kuwaruhusu wanafunzi Mashahidi warudi darasani. Hata hivyo, shule chache zilikataa. Hivyo, Juni 12, 2014, Wizara ya Elimu ilitoa barua iliyotegemeza amri ile iliyopitishwa Septemba 2013 na ikataja sheria mpya inayohusu elimu a ambayo ilipitishwa na Rais wa DRC. Kikumbusho hicho kilishughulikia chanzo cha tatizo hilo kwa kukazia umuhimu wa kupiga vita dhidi ya ubaguzi na kukazia kwamba sheria za taifa na za kimataifa ni muhimu zaidi kuliko sheria za shule. Waziri wa Elimu pia aliteua wakaguzi wa kutembelea shule kotekote nchini humo kuhakikisha kuwa amri hiyo inafuatwa. Bila shaka, hatua hizo za serikali zitakuwa na matokeo mazuri na yenye kudumu.
Faida kwa Wengi
Kadiri shule nchini DRC zinavyoendelea kutenda kupatana na sheria, ndivyo watoto wote wanavyoweza kutarajia kupata elimu bila ubaguzi wa kidini. Watoto wa shule watajifunza kuheshimu watu wote, bila kujali imani yao. Kwa kufanya hivyo, shule nchini DRC hazitakuwa zikifuata tu Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na amri ya Waziri wa Elimu, bali pia zitawawekea vijana wao kielelezo cha kutokuwa na ubaguzi.
a Na. 014/004/2014 “Sheria mpya kuhusu Elimu . . . inawapa wazazi uhuru wa kuwaandikisha watoto wao katika shule yoyote wapendayo. . . . Vita dhidi ya ubaguzi na ukosefu wa usawa ni jambo [muhimu] katika Elimu ya Taifa.”