Hamia kwenye habari

SEPTEMBA 22, 2015
KANADA

Wenye Mamlaka Kaskazini mwa Kanada Washukuru Mashahidi wa Yehova kwa Kampeni ya Pekee ya Kutoa Elimu ya Biblia

Wenye Mamlaka Kaskazini mwa Kanada Washukuru Mashahidi wa Yehova kwa Kampeni ya Pekee ya Kutoa Elimu ya Biblia

TORONTO—Mashahidi wa Yehova 150 hivi walishiriki katika kampeni ya pekee ya kutoa elimu ya Biblia iliyoandaliwa na ofisi ya tawi ya Mashahidi nchini Kanada, mwezi wa Septemba na Oktoba, 2014. Mipango ilifanywa ili kutembelea maeneo 35 ya mbali kotekote nchini.

Zaidi ya watu 32,000 wanaishi katika jamii 35 za watu wa Inuit ambazo Mashahidi walitembelea kama zinavyoonyeshwa na alama za njano. Kampeni ilifanywa katika wilaya mbili na jimbo moja kama inavyoonekana katika rangi ya kijani.

Mashahidi walipangwa katika vikundi na wakaombwa watembelee miji na vijiji vilivyotawanyika katika eneo la Aklavik, Northwest Territories, upande wa magharibi hadi Kangiqsualujjuaq, Quebec, upande wa mashariki, eneo lenye urefu wa kilometa 3,300. Walioshiriki kampeni hiyo walijilipia gharama za usafiri kutia ndani, tiketi za ndege zenye kugharimu dola elfu kadhaa za Marekani kwa mtu mmoja.

Mji mmoja ambao Mashahidi walitembelea ni Paulatuk. Una watu 300 hivi na uko pwani ya Bahari ya Beaufort kaskazini mwa Northwest Territories.

Kabla ya kampeni, Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova liliidhinisha kutafsiriwa kwa video Kwa Nini Ujifunze Biblia? katika lugha ya Inuktitut. Lugha ya Inuit inazungumzwa na watu 35,000 hivi nchini Kanada na inatambuliwa kama lugha rasmi katika eneo la Nunavut na Northwest Territories.

Bi. Velma Illasiak, mkuu wa shule huko Aklavik, alisema hivi kuhusu kampeni hiyo ya Mashahidi: “Wanafunzi walifurahia sana habari mlizozungumzia na wanazifikiria  . . . Tunafikiria kuagiza mabuku mawili ya kitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi kwa ajili ya kila kijana shuleni . . . Asanteni kwa kufika shuleni kwetu na katika jumuia yetu.”

Baada ya kuzungumza na Mashahidi na kutazama video Kwa Nini Ujifunze Biblia?, Bw. Peter Iyaituk, meya wa mji wa Ivujivik kaskazini mwa Quebec, alitumia saa mbili kuwatembeza wageni katika eneo hilo kwa gari lake. Pia aliwapeleka uwanja wa ndege siku waliyoondoka na akawashukuru kwa kuwatembelea.

David Creamore, ambaye ni Shahidi wa Yehova, akimwonyesha meya wa Ivujivik, Bw. Peter Iyaituk, video Kwa Nini Ujifunze Biblia?

Matthieu Rozon, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Kanada, anasema hivi: “Mashahidi wa Yehova wanafurahi kutoa elimu ya Biblia bure kwa kila mtu. Wale walioshiriki walifurahi kwamba walitumia vizuri muda na jitihada zao katika kampeni hiyo.”

Katika kampeni hiyo ya miezi miwili, Mashahidi waligawa machapisho zaidi ya 37,000. Watu 600 hivi waliomba watembelewe na Mashahidi ili waendeleze mazungumzo ya Biblia.

Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:

J. R. Brown, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000

Kanada: Matthieu Rozon, tel. +905 873 4100

 

Uwanja wa ndege wa Kuujjuarapik, Quebec

Kikundi cha Mashahidi kikiwasili Kuujjuarapik, mji ulio upande wa mashariki wa Hudson Bay.

Salluit, Quebec

Mji wa Salluit uko kaskazini mwa Quebec na una wakazi zaidi ya 1,300.

Ivujivik, Quebec

Mji wa Ivujivik uko pia kaskazini mwa Quebec na una idadi ya watu 400 hivi.

Ivujivik, Quebec

David Creamore akitembezwa mjini na meya wa Ivujivik, Bw. Peter Iyaituk.

Ivujivik, Quebec

Kijana wa Inuit akitazama video Kwa Nini Ujifunze Biblia?

Paulatuk, Northwest Territories

Nyumba za watu zimefika hadi kwenye Bahari ya Beaufort Sea katika eneo jembamba la mji huo wenye watu 300 hivi.

Umiujaq, Quebec

Wenzi wa ndoa wa Inuit wamemwalika nyumbani Julien Pinard, Shahidi mmojawapo aliyetembelea eneo hilo, ili wazungumzie Biblia. Mji huo una karibu watu 450.

Umiujaq, Quebec

Wakazi wa mji huo ulio kaskazini mwa Quebec wakiwa wamesimama kupiga picha na Roxanne Pinard (kulia), mmojawapo wa Mashahidi waliotembelea eneo hilo.

Puvirnituq, Quebec

Watu 1,700 hivi wanaishi katika kijiji hiki kilichopo kaskazini mwa Quebec.