OKTOBA 13, 2017
KAZAKHSTAN
Kazakhstan Imepatikana na Hatia ya Kumfunga Isivyo Haki Teymur Akhmedov
Kikundi cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Vifungo Vilivyo Kinyume cha Sheria (WGAD) kimeilaumu serikali ya Kazakhstan kwa kumfunga Teymur Akhmedov na wameagiza aachiliwe mara moja. a Katika uamuzi wake uliochapishwa Oktoba 2, 2017, WGAD ilisema kwamba serikali ya Kazakhstan ina hatia ya kumfunga isivyo haki Bw. Akhmedov, ambaye amekuwa kifungoni tangu Januari 18, 2017, kwa sababu ya kuwaeleza watu wengine imani yake kwa amani.
Uamuzi wa WGAD
Katika uamuzi wake, WGAD ilisema kwamba Bw. Akhmedov amefungwa isivyo haki. WGAD imetambua kwamba serikali imemnyima uhuru wa kutimiza haki yake ya msingi ya uhuru wa ibada na kujieleza, kesi yake haikuendeshwa kwa haki na usawa, na kubaguliwa kwa sababu tu ya utendaji wa kidini akiwa Shahidi wa Yehova.
WGAD inaishutumu Kazakhstan hasa kwa kumkamata isivyo haki na kumshitaki Bw. Akhmedov. Ilirejelea uamuzi wa awali wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu ambao uliipinga serikali ya Kazakhstan kwa sababu “ya kuunda sheria isiyo wazi ya ‘msimamo mkali’ . . . na kuitumia sheria hiyo ya msimamo mkali kuzuia sana uhuru wa ibada, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa kukusanyika na kushirikiana.” WGAD ilieleza kwamba sheria hiyo “inatishia sana uhuru wa ibada nchini Kazakhstan” na kwamba “kesi hii ya Bw. Akhmedov ni uthibitisho dhahiri wa tishio hili.”
Lakini WGAD imeeleza mara kadhaa kwamba utendaji wa kidini wa Bw. Akhmedov ni wa “amani kabisa” na ilieleza kuwa mazungumzo ya kidini aliyofanya pamoja na wengine hayakuhusisha kuchochea vurugu au chuki ya kidini. WGAD imekazia kwamba serikali “haikutoa mfano wowote wa tukio la jeuri au pindi ambayo Bw. Akhmedov amewachochea wengine wafanye vurugu” na serikali “haijaeleza jinsi kukutana tu na wengine na kuzungumza nao kwa amani mambo ya kidini ni kosa la uhalifu.” WGAD ilisema hivi pia: “Ni dhahiri kwetu kwamba Bw. Akhmedov alikuwa akitimiza haki yake ya uhuru wa ibada ambayo inaelezwa katika kifungu cha 18 cha Mkataba.” b
Kwa kuongezea, WGAD inahusianisha jinsi serikali ilivyomtendea Bw. Akhmedov pamoja na uthibitisho mwingine wa ubaguzi wa kidini kuwa sehemu ya ushahidi wa wenye mamlaka nchini Kazakhstan kuwashambulia Mashahidi wa Yehova. Ukweli wa jambo hilo ulithibitishwa wenye mamlaka walipovamia jengo la ibada la Mashahidi na kupora machapisho ya kidini siku ileile ambayo Bw. Akhmedov alikamatwa.
“Ni dhahiri kwa WGAD kwamba Bw. Akhmedov alikuwa akitimiza haki yake ya uhuru wa ibada ambayo inaelezwa katika kifungu cha 18 cha Mkataba.”—Maoni, ukurasa wa 39.
Wenye Mamlaka Nchini Kazakhstan Wanapaswa Kuchukua Hatua
WGAD inaiomba Kazakhstan “ichukue hatua zinazofaa ili kurekebisha hali ya Bw. Akhmedov bila kuchelewa.” WGAD ilieleza kwamba marekebisho yanayofaa “ni kumwachilia Bw. Akhmedov mara moja na kumpa haki ya kupata fidia na haki nyingine.” Pia, WGAD inaiomba Kazakhstan ibadili sheria na mazoea yake ili ijipatanishe na matakwa ya kimataifa, ambayo yataisaidia isirudie tena kosa kama walilomfanyia Bw. Akhmedov.
Oktoba 13, 2017, mawakili wa Bw. Akhmedov walikata rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Kazakhstan, wakiomba mahakama hiyo itekeleze uamuzi wa WGAD, kumwondolea mashtaka, na kuamuru atolewe mara moja.
Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote wanafurahi kwamba kesi ya Teymur Akhmedov imetambuliwa na ulimwengu mzima kuwa si ya haki na inaonyesha uhitaji mkubwa wa kuheshimiwa kwa uhuru wa ibada nchini Kazakhstan. Wanatumaini kwamba serikali ya Kazakhstan itatekeleza uamuzi wa WGAD na kumwachilia mara moja Bw. Akhmedov kutoka gerezani.
a Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu, Mapendekezo yaliyotolewa na Kikundi Kinachoshughulikia Vifungo Visivyo vya Haki katika sehemu ya 79: Na. 62/2017, Kazakhstan, U.N. Doc. A/HRC/WGAD/2017/62 (Agosti 25, 2017).
b Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa